Breaking

Friday, 11 November 2022

DKT. KIRUSWA ATATUA MGOGORO WA MWEKEZAJI NA WANANCHI BUTIAMA



Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amefungua Kikao cha kutatua mgogoro baina ya mwekezaji mgodi wa Cata Mining na jamii inayozunguka mgodi huo baada ya malalamiko kuhusu ulipwaji wa fidia kwa wananchi waliyopisha eneo la uwekezaji.

Mgodi wa Cata Mining uliopo wilayani Butiama mkoa wa Mara unashutumiwa kwa kuchelewesha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Aidha, Dkt. Kiruswa amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Madini, suala la kuchangia huduma kwa jamii inayozunguka leseni ya mgodi ni jambo la kisheria na sio msaada kwa jamii, hivyo ameitaka Kampuni ya Cata Mining kuchangia huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo kwa mujibu wa Sheria.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameiagiza Kampuni ya Cata Mining kutekeleza takwa la kuchangia huduma kwa jamii inayozunguza mgodi pamoja na kulipa fidia kwa walio pisha eneo la mgodi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee ameahidi kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha jamii inayozunguka mgodi huo inapata haki yake na mwekezaji anaye miliki leseni ya eneo hilo anachangia huduma kwa jamii.

Pia, Kaimu Kamishna wa Madini Msechu Mwaluvoko amasema, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, kifungu cha kumtaka mmiliki kiliongezwa kwa msisitizo kifungu namba 105 kiliongezwa kusisitiza mmiliki wa leseni kuchangia huduma kwa jamii zinazozunguka mgodi.

Amesema upo mwongozo wa kuchangia huduma kwa jamii inayo zunguka mgodi ambao unamtaka mwekezaji kuandaa mpango wa kuchangia huduma kwa jamii inayo zunguka mgodi na kuiwasilisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya mapitio na baadaye utekelezaji.

Kikao hicho, kimehudhuliwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Madini Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu Madini Msafiri Mbibo, Kaimu Kamishna wa Madini Msechu Mwakavuko, Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Moses Kaegele, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama Patricia Kabaka pamoja na Madiwani wanao hudumu katika maeneo yanayozunguka mgodi huo wakiongozwa na Rajabu Mjengwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages