MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amesema katika tukio ambalo limetokea jana la bwawa la mgodi wa almasi mwadui kubomoka na kusambaza tope kwenye makazi ya watu, kuwa hakuna kifo ambacho kimetokea zaidi ya mashamba na baadhi ya Kaya kuathirika, huku Mgodi huo ukisimama kwa muda kufanya shughuli za uzalishaji Almasi.
Tukio hilo la bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui la kuhifadhia maji machafu kubomoka lilitokea jana majira ya saa 4 asubuhi, ambapo baadhi ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo vilipata madhara kiasi ikiwamo kuharibika mashamba na visima vya maji kufunikwa na tope.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, amesema watu walioathirika na tukio hilo ni 59, nyumba 13 zimezingirwa na tope, huku watoto watatu wakipata tatizo la kutapika na wameshapelekwa hospitali kupatiwa matibabu.
Amesema vijiji ambavyo vimeathiriwa zaidi na tope hilo ni Ng’wang’oholo, na Nyeze ambapo nyumba zao na mshamba zimeathiriwa zaidi na tope la mgodi huo, na tayari wameshapelekewa msaada wa chakuna na maji, huku Serikali ikiendelea kufanya tathimini ya tukio hilo.
“Mgodi wa Mwadui jana ulipata tatizo la bwawa lake kubomoka na kusambaza tope kwenye makazi ya watu, lakini tunashukuru hakuna kifo hata kimoja na mgodi umesimama kwa muda kufanya shughuli za uzalishaji Almasi hadi pale tutakapo jiridhisha kuwa kuna usalama,”amesema Mjema.
“Nyumba ambazo zimezingirwa na tope ni 13, na wananchi walioathirika ni 59 na Kaya 19 na watoto watatu walipata shida kidogo ya kiafya na wanaendelea na matibabu, na Serikali tumeshaunda tume ambayo inachunguza tukio hilo na itakuja na majibu yote pamoja na kutoa tathimini ya ujumla,”amesema Mjema.
Aidha, akizungumzia juu ya madhara ya udongo huo kwa binadamu, amesema uchunguzi tayari unafanyika ambapo sampuli zimeshachukuliwa, ili kuona kama kuna madhara yoyote ya binadamu.
Via: Shinyanga Press Club Blog