Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 48, anapokea matibabu baada ya kushambuliwa na kulawitiwa na genge lisilojulikana katika Kituo cha Nderu eneo la Ndeiya, Kaunti ya Kiambu nchini Kenya.
Uchunguzi umebaini kuwa mwanaume huyo ambaye ni mlemavu, alivamiwa alipokuwa kwa matembezi ya jioni katika eneo la Ndeiya, lililoko kati kati ya kaunti ndogo za Limuru na Kikuyu.
Wakazi waliohojiwa na Citizen TV, walisema kwamba mwathiriwa alibanwa na majangili hao muda mfupi baada ya kuondoka katika baa moja ya eneo hilo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mwathiriwa alilawitiwa na wavamizi hao kisha kumkata sehemu zake za siri.
"Tunashuku kuwa kinywaji cha mwathiriwa kilikuwa na dawa za kulevya. Ni lazima washukiwa walitumia dawa ya kumlewesha kabla ya kumtupa barabarani. Inasikitisha," mkazi mmoja alisema.
Kitendo hicho cha kinyama kimewaghadhabisha sana wenyeji wakitaka hatua za haraka kuchukuliwa na mamlaka husika.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Ndeiya, Roseline Mnyolmo alisema wanafanya uchunguzi ili kuwakamata wahusika wa kitendo hicho kiovu na kuwashtaki.
Kwa sasa mwathiriwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kiambu Level Five baada ya kupokea huduma ya kwanza katika Hospitali ya Ndeiya Level Three.