Breaking

Monday, 24 October 2022

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAAHIDI KUONGEZA NGUVU KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII VYA TANZANIA



Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuwa Wizara anayoiongoza inaendelea kuongeza nguvu katika kutangaza utalii na vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia maonesho na mikutano mikubwa ya Kimataifa ukiwemo ule wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika [UNWTO-CAF] uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha na Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili 'Swahili International Tourism Expo' (SITE) lililofanyika jijini Dar es salaam.

Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2022 jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu utekelezaji wa kazi mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika Sekta ya Maliasili na Utalii.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi kubwa inayofanya ya kuisimamia Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akiishukuru Kamati hiyo kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa Wizara na kubainisha kuwa Wizara anayoiongoza itaendelea kuufanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati hiyo ili kuendeleza sekta ya Maliasili na Utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Juma Ally Makoa (Mb) amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikifanya vizuri katika kulinda,kuhifadhi na kuendeleza maliasili zilizopo hapa nchini ili ziendelee kuwanufaisha Watanzania wote.

“ Kamati inaridhishwa na kutiwa moyo na juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara katika Kuhifadhi, kulinda na kuendeleza maliasili. Mhe. Waziri mimi kama Mwenyekiti wa Kamati nakupongeza, jana ulikua Moshi kwenye tukio la kuzima moto Mlima Kilimanjaro na leo umekuja kwenye Kamati” Amesisitiza Mhe.Makoa

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof . Eliamani Sedoyeka amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Kamati hiyo na kuyafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na Kamati ili kuhakikisha sekta ya utalii hapa nchini inaendelea kuimarika.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages