Na John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwa wenyeji na kuandaa mashindano ya 12 ya Dunia ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa viziwi ambayo mtanzania Hadija Kanyama ametwaa taji la Urembo la Dunia Kwa viziwi.
Mhe Rais ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter "Nakupongeza Hadija Kanyama kwa kutwaa taji la Urembo la Dunia kwa viziwi. Ushindi huu ni heshima kwa nchi yetu na nakutakia kheri katika majukumu yako."
Aidha, Mhe Rais amemtaka Kanyama kuendelea kuelimisha jamii kutowaficha na kuwapa nafasi wenye Ulemavu.
Mara baada ya ushindi huo hapo jana, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa aliwapongeza washiriki wa Tanzania kwa kufanya vizuri na kutwaa ubingwa kwenye shindano hilo ambapo pia mtanzania, Rajan Ally alikuwa mshindi wa pili wa taji la Utanashati wakati, Russo Songoro akishinda taji la wanaume upande wa Mitindo.
Alisema tamasha hili ni miongoni mwa matamasha makubwa duniani ambalo limeiheshimisha Tanzania na alimshukuru, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuamsha ari na kuinua vipaji vya watanzania na sasa vinaonekana na kuitangaza Tanzania dunia.
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais, tunawapongeza watanzania wote kwa kuwa ushindi huu ni wa watanzania wote kwa ujumla na hii ndiyo tafsri ambayo Mhe. Rais amekuwa akitamani kuionyesha na kuwataka watanzania waionyeshe na kuonyesha vipaji vyao.” Ameongeza Mhe. Mchengerwa
Mshindi wa pili kwa upande wa Miss ni Chanika Vilioen kutoka Afrika Kusini wakati mshindi wa tatu ni Miseon Kang kutoka Korea kusini.
Kwa upande wa Mister, Mu-Australia Gareth Kelaart ametwaa taji hilo akifuatiwa na mtanzania Rajani Ally na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Hung Nguyen kutoka Vietnam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari siku moja kabla ya shindano hilo, Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt Hassan Abbasi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya kutangaza vivutio vya Utalii nchini - Royal tour alieleza kuwa kesho Oktoba 31, 2022 Serikali imetoa zawadi kwa washindi wa makundi yote na viongozi kutembelea mbuga ya Ngorongoro ili kujionea utajiri wa vivutio vya Utalii vilivyopo nchini.
Ziara hiyo itasaidia pia kwa washindi hao kuwa mabalozi wazuri wanapprejea katika nchi zao.