Na WMJJWM Arusha
Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Bi. Mwantumu Mahiza ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwekaza nguvu zaidi kwenye Mikoa ambayo inawadau wa chache wanayoshughulikia afua za watoto pamoja na kuepuka kurundikana kufanya kazi katika eneo moja la nchi na kuiacha mikoa mingine ikikosa usaidizi wa wadau.
Bibi Mwantumu ameyasema hayo wakati wa kikao kilichofanyika jijini Arusha kikijumuisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayoshughulikia masuala ya watoto yakiwemo Mashirika ya Pact Tanzania, SOS, Compassion na Plan International.
Amesema kuwa lengo la kikao hicho, ni kufanya majadiliano ya kina kuhusu utendaji kazi wa Mashirika na mchango wao kwa jamii hususan katika utatuzi wa changamoto zinazowakumba watoto nchini kama vile; kukithiri kwa vitendo vya ukatili nchini wanavyofanyiwa Watoto na ongezeko la watoto wa mitaani kwenye Miji na Majiji lakini pia kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Amefafanua kuwa kutokana na baadhi ya viongozi na Mamlaka za Serikali nchini kutokuwa na taarifa za kina kuhusu kazi zinazofanywa na NGOs, na kuzitaka NGOs zihakikishe zinashirikisha kikamilifu Mamlaka za Serikali kwenye maeneo wanayotekeleza miradi.
"Niyatake Mashirika Yasiyo ya Kiserikali waongeze kasi ya utumiaji vyombo vya Habari kutangaza kazi zao wanazozifanya" alisema Bibi. Mwantumu
Aidha Bibi Mwantumu ametoa rai kwa Wizara za kisekta zinazoshughulikia afua ya Watoto kama vile Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuboreshe mifumo ya uratibu wa pamoja katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto.
Kwenye maazimio hayo yaliyofikiwa, Mashirika hayo pia yalipata fursa ya kupaza sauti ya pamoja ya kuendelea kupinga ukatili unaoendelea kufanywa kwa watoto ikiwemo kuandaa jumbe za njia ya simu, zinazomkumbusha mzazi/mlezi kujenga urafiki wa kuongea au utamaduni wa kumsikiliza mtoto, kuandaa maandamano ya amani yenye ujumbe wa kupinga ukatili nchini.
MWISHO