Breaking

Wednesday, 26 October 2022

WATU WATATU WAUAWA WAKIWEMO ASKARI WA UHAMIAJI -GEITA






Watu watatu wakiwepo askari wawili wa Jeshi la Uhamiaji na mwananchi mmoja wameuawa katika kijiji cha Mtakuja, Kata ya Lulembela, Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita tarehe 26.10.2022 majira ya saa nane usiku.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la polisi nchini SACP David Misime ameeleza kuwa Mauaji hayo yametokea usiku wa Kuamkia leo Jumatano Oktoba 26, 2022 majira ya saa nane usiku.

Amewataja waliouawa kuwa ni Mkaguzi wa Jeshi la Uhamiaji Salum Msongela Mpole na Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Gilbert Edward, wote kituo Chao cha kazi ni wilaya ya Bukombe na eneo la Mbogwe likiwa chini yao pia.

"Mwananchi aliyeuawa anajulikana kwa jina la Juma Bundala wa kijiji hicho cha Mtakuja" Ameeleza SACP Misime

Aidha, askari mmoja konstebo wa uhamiaji amejeruhiwa katika tukio hilo na amelazwa hospitali akiendelea na matibabu.

SACP Misime amesema kuwa chanzo cha tukio hilo la mauaji ya kujichukulia sheria mikononi kinadaiwa ni baada ya askari hao kufika katika kijiji hicho baada ya kupata taarifa za uwepo wa wahamiaji haramu katika nyumba ya mwananchi mmoja kijijini hapo.

Hadi sasa watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na tukio hilo.

"Timu ya uchunguzi imeshatumwa kwenda katika kijiji hicho, kufanya uchunguzi wa mazingira yote yanayozunguka tukio hilo ili hatua ziweze kuchukuliwa kulingana na ushahidi utakaokusanywa na timu hiyo." Imeeleza taarifa

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Mtakuja kuwa watulivu na kufuata sheria wakati wa uchunguzi ukiendelea.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages