Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Mohamed Mchengerwa amesema shindano la Dunia la utanashati, urembo na mitindo kwa watu wenye matatizo ya usikivu litafanyika Oktoba 29, 2022 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, jana Mhe. Mchengerwa amesema maandalizi yote yamekamilika na tayari wageni kutoka mataifa mbalimbali wameshawasili tayari kwa mashindano hayo.
Mtendaji Mkuu wa Shindano hilo Duniani, Bonita Annleek amesema Tanzania ilipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa shindano hilo kutokana na rekodi ya Amani na vivutio vya Utalii, ukarimu na Ushirikiano na nchi nyingine.
Aidha, Tanzania mwaka jana ilikuwa mwenyeji na kupata mafanikio kwenye shindano hili kwa ngazi ya Bara la Afrika.
Hadi sasa tayari kambi ya kutafuta mshindi inaendelea kwenye hotel ya Peackok jijini Dar es Salaam.
Tanzania inawakilishwa na washiriki sita ambao niKhadija Kanyama, Joyce Dennis,Carlyone Mwakasaka, Durath Mwarkis, Rajabu Ally na Russo Songoro.
Washiriki hao wamesisitiza kuwa wamefanya mazoezi ya kutosha na wataipeperusha vema bendera ya Tanzania.
Tayari washiriki wa Tanzania walianza mazoezi ya kujinoa kwa ajili ya mashindano hayo toka mwezi Agosti mwaka huu kwenye Chuo cha Sanaa na Utamaduni (TaSUBa)