Na John Mapepele
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imempongeza kwa mchango wake, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Wizara Katika Maboresho ya Michezo, Sanaa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo ameyasema hayo Oktoba 25, 2022 baada ya kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa
"Waheshimiwa wajumbe wa Kamati sasa kwa hili naomba Kwa heshima nisimame na kusema kuwa mafanikio haya yote tunayoyapata kwenye mashindano ya Kombe la Dunia ni kutokana na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwenye michezo" amefafanua Mhe. Nyongo
Amemwomba Waziri Mchengerwa kuzileta timu za Taifa za soka za Serengeti girls na Tembo Warriors kuzileta bungeni ili zipewe pongezi mara baada ya kupambana na kuandika historia ya kuwa timu pekee kufika katika robo fainali za mashindano ya Kombe la Dunia.
Aidha ameipongeza uongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwa wabunifu ambapo amefafanua kwamba Wizara kwa sasa imekuwa inaonekana ukifanya vizuri kuliko awali
Akiwasilisha taarifa hiyo Waziri Mchengerwa amesema Chuo cha Michezo cha Malya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinakwenda kufanya utafiti kuhusu mchango wa michezo kwenye maendeleo ya uchumi nchini ili kuweza kuishauri Serikali namna bora ya kuifanya michezo ichangie kikamilifu kwenye uchumi wa nchi.
Amesema katika hatua ya kuimarisha michezo nchini, Serikali ya awamu ya Sita inayoongongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samaia Suluhu Hassan inatekeleza miradi mbalimbali katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ikiwemo ujenzi wa Hosteli yenye ghorofa nne, ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kukuzia na kuendeleza vipaji vya michezo na uchimbaji wa kisima cha kisasa cha maji.
Aidha, amesema tayari Wizara imevielekeza vilabu vyote vya michezo kuwasilisha mipango ya kujenga viwanja kulingana na Sera ya Michezo ambapo amesema alitoa miezi sita ambapo amefafanua imebaki miezi mitatu.
Amesema dhamira ya sasa ya Serikali ni kukarabati viwanja 5 vya Mwanza, Dodoma, Tanga, Arusha na Mbeya ambapo gharama yake ni takribani bilioni 70 ili Tanzania ifuzu vigezo vya kuandaa mashindano ya AFCON 2027.
Amesema, Wizara inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kutafuta fedha kutoka kila sehemu ili kuweza kufanya ukarabati wa miundombinu kutokana na ufinyu wa Bajeti.
Akitolea mfano amesema bajeti kwa ajili ujenzi kwa wa miundombinu yote ya Chuo cha Michezo cha Malya ni Bilioni 52 ambapo amesema hadi sasa tayari Serikali imeshatoa zaidi ya milioni mia tano.
Wabunge wameomba kuanzisha tawi la chuo cha Malya upande wa Zanzibar ambapo Mhe. Mchengerwa amekubali kulifanyia kazi.