Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
IKIWA Tanzania ikiadhimisha miaka 23 tokea kifo Cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Jukwaa la Magomeni Huru limemuenzi kwa aina yake kwa kufanya usafi kwenye Makaburi ya Ndugumbi na kudhuru Makumbusho yake yaliyopo Magomeni eneo la Usalama.
Mratibu wa shughuli hiyo, Bw. Sadique Bwanga amesema Jukwaa la Magomeni Huru linajumlisha Wajumbe mbali mbali wakiwemo wadau ambao ni viongozi wa Kisiasa na kijamii kote nchini.
"Hii ni mara ya kwanza tunafanya tukio hili katika kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Nyerere, tumejumuika kwa pamoja katika kudumisha tunu ya umoja aliyotuachia, lakini pia katika kuunga mkono masuala mazima ya utalii wa ndani, tumetembelea makazi yake aliyokuwa akiishi pale Magomeni eneo la Usalama, yote haya ni katika kuungana na Watanzania wote kwenye maadhimisho ya siku hii ya Nyerere (Nyerere Day)." Amesema Sadique Bwanga
Aidha, amesema kuwa jukwaa la Magomeni Huru lina watu mbalimbali na limekuwa likifanya shughuli za kijamii, Siasa, Michezo na mengine mengi katika kuleta Maendeleo kwa Taifa" amesema Sadique Bwanga.
Aidha, tukio hilo la ufanyaji usafi ni la pili kwani pia wamekuwa wakijumuika pamoja na Wananchi katika ufanyaji wa usafi kwenye mitaa mbalimbali ndani ya Magomeni.
Katika tukio hilo viongozi mbalimbali wameweza kujumuika kwa pamoja na Magomeni Huru akiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam-CCM, Idd Azan, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Bw Shaweji Mkumbura, na wengine wengi wakiwemo wenyeviti wa matawi na vikundi vya mazoezi (Jogging) vilivyopo Magomeni.
Mwisho.