Breaking

Saturday, 22 October 2022

BRELA, FCC, TIC, WAKUTANA NA WADAU




Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kupitia Taasisi zake za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Kituo Cha Uwekezaji (TIC), wamekutana na wadau mbalimbali kutoka katika taasisi za umma na binafsi katika kikao cha mashauriano kuhusu Itifaki za Ushindani, Uwekezaji na Haki za Miliki Ubunifu, chini ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).


Kikao hicho kimefanyika Oktoba 21, 2022 katika ofisi za FCC zilizopo Dar es Salaam na kupitia kwa pamoja Itifaki hizo zinazolenga kusimamia na kuwezesha ufanyaji biashara kwa nchi wanachama wa Soko huru la Afrika.


Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Bw. Ally Gugu, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mtangamano wa Biashara wa Wizara hiyo Bw.Ombeni Mwasha amesema, mchakato wa kuanzishwa Soko la pamoja utakapo kamilika utakuwa na manufaa mengi kwa taifa la Tanzania.


Bw. Mwasha amesema taifa la Tanzania limebarikiwa jiografia na ni rafiki kwa Uwekezaji hivyo wadau ni wajibu wao kutoa mchango wa mawazo ili kuandaa Itifaki zitakazoleta manufaa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa FCC Dkt. William Erio akitoa neno la ukaribisho kwa wadau waliofika katika kikao hicho amesema mwitikio wa wadau katika kikao hicho unatoa mwanga kuwa yale yatakayojadiliwa yatakuwa yenye tija na kazi hiyo itakuwa nyepesi katika kukamilisha mchakato.



Naye Msajili Msaidizi Mkuu kutoka BRELA Bi. Loy Mhando, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa, amesema kikao hicho ni muhimu kwa Taifa na Afrika kwa ujumla kwani kinalenga kutengeneza mazingira rafiki ya ufanyaji biashara katika Eneo Huru la Biashara Afrika ambapo Itifaki hizo ni moja ya suala linalopaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu, ili utekelezaji wake utakapoanza wadau waweze kunufaika na bunifu zao pamoja na kuwezesha ufanyaji biashara.


"Itifaki hizo za Miliki Ubunifu ni lazima zipitiwe na kuboreshwa ili utekelezaji wake uwe ni wenye manufaa Kwa wabunifu na taifa Kwa ujumla," amefafanua Bi. Mhando na kuongeza kuwa yapo maeneo muhimu ambayo tayari yamekwisha jadiliwa na kupatiwa muafaka katika vikao vilivyopita.



Ameongeza kuwa katika baadhi ya maeneo maoni ya wadau yanahitajika na mjadala wa pamoja, ili kuboresha zaidi na kupata Itifaki bora.


"Hapa mpo wanasheria, wataalam, pamoja na wadau ambao kwa pamoja tukishauriana tutatoka na muafaka na jambo hili litafanikiwa," amesema Bi. Mhando.


Ameongeza kuwa Eneo Huru la Biashara litachochea ukuaji wa uchumi, hivyo ni vyema sera na mipango itakayopitishwa iwe ni yenye kugusa maisha ya watu na kuwezesha ufanyaji biashara barani Afrika.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miungano ya Makampuni,Tafiti na Ushawishi wa Ushindani wa FCC Bi. Zaytun Kikula amewataka wadau kuchangia mawazo yao katika kuboresha chapisho la Itifaki za Ushindani katika Eneo Huru la Biashara Afrika ili kuchochea Ushindani wenye manufaa.


Wadau kwa pamoja wametoa maoni yao katika masuala mbalimbali ya Itifaki husika ambayo yamefanyiwa mabadiliko ili kuleta muafaka ambao utakuwa na tija katika ufanyaji Biashara katika Eneo Huru la Biashara Afrika.


Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 wanachama kati ya nchi 55 za Afrika zilizosaini makubaliano ya kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara Afrika, ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama wa Afrika.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages