Polisi katika eneobunge la Kiminini, kaunti ya Trans Nzoia, nchini Kenya wanamsaka kijana mwenye umri wa miaka 21, Brian Wafula, ambaye anashukiwa kumuua mama yake Judith Nafula Konya.
Nafula, ambaye alikuwa akihudumu katika maabara ya Shule ya Wasichana ya St Joseph's Kitale, alitoweka siku ya Jumanne, Oktoba 18, katika hali isiyoeleweka.
Mwili wa marehemu mwenye umri wa miaka 50, baadaye ulipatikana ukielea kwenye Mto Kiminini jioni ya Jumamosi, Oktoba 22.
Kabla ya kutoweka kwake, inaripotiwa kuwa Nafula alizozana na mwanawe baada ya kuuza baadhi ya mazao ya shambani bila idhini yake.
Kufuatia kuzozana huko, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kiminini John Onditi alisema kuwa mshukiwa alitishia kumuua mama yake.
Kisha alitoweka hadi Jumamosi wakati mwili wake uliopolewa kutoka kwenye Mto Kiminini na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Wafula pia alitoweka siku hiyo hiyo mama yake aligunduliwa hayupo.
Mwili wa Nafula ulikuwa na majeraha na sasa uchunguzi wa maiti utafanywa ili kubaini chanzo cha kifo chake.
Mume wake, Andrew Wanjala Wekesa, alisimulia kwa uchungu kwamba alikuwa amemjulisha kuhusu kutishiwa maisha na mwana wao Wafula.
Wekesa alisisitiza kuwa mtoto wao ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji hayo kwani begi lake lilikuwa na vitu vinavyomhusisha na kifo hicho, zikiwemo funguo za nyumba yao kuu.