Polisi nchini Uganda wanachunguza chanzo cha moto katika shule ya bweni ya wanafunzi wenye ulemavu wa macho ulioua wasichana 11 wenye umri wa miaka minne hadi 13.
Moto katika Shule ya Wasioona ya Salama katika wilaya ya Mukono ya kati nchini Uganda ulizuka muda mfupi baada ya saa sita usiku Jumatatu, katika bweni la wasichana ambalo lilikuwa na watoto 17.
Naibu msemaji wa polisi wa Kampala Luke Owoyesigire alisema polisi wametuma timu ya uchunguzi wa kitaalamu ambayo itafanya uchunguzi wa DNA kabla ya miili ya watoto waliokufa kukabidhiwa kwa wanafamilia.
"Chanzo cha moto huo kwa sasa hakijajulikana. Lakini kufikia sasa, vifo kumi na moja vilivyosababishwa na moto huo vimethibitishwa. Huku sita wako katika hali mbaya," Owoyesigire alisema.
Shule ya Wasioona ya Salam, iliyoko katika mji wa Kisoga, ina watoto 70 wenye ulemavu wa macho.
Hudson Kiyaga, meya wa mji huo, aliiambia VOA moto katika shule iliyotengwa umewaacha watu wa jamii jirani na mshangao. Kiyaga alisema swichi ya umeme ya shule hiyo ipo kwenye chumba cha matroni, lakini hajui kilichoanzisha moto huo. Matron aliepuka moto huo, lakini hakuweza kuokoa mwanafunzi yeyote.
Mjumbe wa bodi ya shule hiyo, Charles Nkuse, alisema mwalimu mkuu wa shule alimpigia simu saa 12:15 asubuhi na kumweleza kuwa shule inateketea kwa moto na watoto wamefariki dunia.
Moto huo ulizuka siku chache tu kabla ya ziara iliyopangwa ya Princess Anne wa Uingereza na mke wa rais wa Uganda, Janet Museveni.
"Tunatarajia kupata mwanamke wa kwanza, binti wa marehemu Malkia, Princess Anne, na mume. Walipaswa kuwa nasi siku ya Ijumaa, lakini kwa kweli sijui nini kitafanyika," Nkuse alisema. "Lakini, bado tuko katika hali mbaya kwa sababu, nadhani, polisi wanarudisha maiti kutoka Mulago na wazazi wako hapa."
Tangu Januari, shule kadhaa nchini Uganda zimeshika moto lakini maafisa wa usalama bado hawajabaini chanzo cha moto huo.
Katika miongozo yake kwa shule, Wizara ya Elimu inashauri kwamba mabweni yote miongoni mwa majengo mengine ya shule yawe na vizima-moto katika maeneo kadhaa. Walakini, shule nyingi hazina hatua kama hizo za usalama.