Francis Banda, mwanamume kutoka Malawi anayeishi Ntcheu, anagonga vichwa vya habari baada ya kubomoa nyumba mbili kutokana na hasira iliyosababishwa na kuvunjwa moyo.
Malawi 24 inaripoti kuwa mke wake Banda alimwacha na kukimbilia kwa mwanamume mwingine, jambo ambalo lilimuumiza sana moyo hadi kumchochea kubomoa nyumba aliyomjengea pamoja na mama mkwe wake.
Kulingana na kanda ya sauti iliyotolewa, Banda alikuwa ameoana na mkewe kwa miaka 13 na wana watoto watatu.
Alifichua kwamba wakati wa ndoa yao, alijikakamua na kujenga nyumba mbili; moja ya mke wake na nyingine kijijini ya mama mkwe wake.
Licha ya bidii yake, mke wake Banda aliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine na hivi majuzi alihamia kwake.
"Wakati fulani, nilijaribu kuwasiliana na mke wangu lakini simu yake ilipokelewa na mpenzi wake," Banda alisema.
Hapo ndipo hasira yake ilipanda na ikampelekea kwenda kuziharibu nyumba mbili alizozijenga.
Wananchi waliopata habari kuhusu matendo yake walimtaja mke wake wa zamani kama mtu asiyekuwa na shukurani na walisema wanaelewa uamuzi wa mwanamume huyo.