Breaking

Friday, 21 October 2022

WORLD VISION YATOA VIFAA VYENYE THAMANI MILIONI 152 SHULE ZA MSINGI UYUI



Na Lucas Raphael,Tabora

SHIRIKA la World Vision Tanzania kupitia wafadhili kutoka nchini ya Japan wametoa Madawati 590 , Madaftari 3200,Kalamu za wino 2500, Penseli 730 na sare 600 za wanafunzi, kwa wanafunzi wa shule za msingi vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 152.9 .

Akizungunza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo Mkuu wa wilaya ya Uyui,Kisare Makori alisema kuwa licha ya serikali kufanya kazi kubwa katika sekta ya elimu na afya lakini bado haijatosheleza hivyo kuwepo kwa wadau wa maendeleo kama vile shirika hilo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii .

Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imeweza kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita hivyo ameitaka jamii kulinda miundo mbinu ya shule inayoletwa na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kama vile shirika la World Vission ili iweze kusaidia watoto .

"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu inafanya kazi kubwa sana katika nyanja zote ikiwemo ya elimu tumeshuhudia sasa elimu ya msingi hadi kudato cha sita kwa sasa inatolewa bila malipo na miundo mbinu inajengwa hivyo niwaombe wananchi tunzeni hii miundombinu iliyojengwa na serikali na ile iliyoletwa na wadau wetu wa maendeleo wakiwemo World Vision,"alisema Makori.

Naye Meneja wa World Visio Kanda ya Nzega,Jacqueline Kaihura alisema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zenye lengo la kuibadilisha jamii katika kuboresha afya ya mtoto na mazingira ya kusoma na kujifunza katika shule za msingi .

Alisema kuwa wamebaini ya kuwa katika kijiji cha Mwisole kuna changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hivyo katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango huo moja ya kazi waliyopanga ni kuchimba kisima kirefu cha maji kitakachogharimu kiasi cha Shilingi 130 ili wananchi waweze kupata maji safi na salama.

“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali sisi pamoja na wafadhili wetu wa Japan kuwa ni sehemu ya kuchochea maendelo kwa wananchi wetu hapa nchini natumaini kwa miaka 12 ijayo tutakayokuwepo kwenye eneo hili la Lutende nikuhaidi Mkuu wa wilaya tutafanya kazi kwa weledi mkubwa ili tuweze kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta zote ambazo tutazigusa hivyo wananchi waendelee kutupatia ushirikiano,"alisema Jacqueline.

Mratibu wa Lutende AP, Michael Ngasa wakati akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka wa fedha 2021/2022 wa Mpango huo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Uyui,Kisare Makori alisema kwamba wametoa kadi ya Bima za Afya iliyoborea kwa watoto 500 na vyeti vya kuzaliwa 208 kwa watoto waliozidi miaka mitano hasa wale waliotambuliwa kuwa na magonjwa sugu kama vile Selimundu ambao watapata fursa ya matibabu katika Hospitali za Rufaa kupitia uwezeshi wa shirika hilo sambamba na kutoa mafunzo ya lishe bora kwa watoto.

Alisema kuwa mradi huo ambao ni wa miaka 12 katika eneo hilo lenye vijiji vya Lutende,Mwisole,Itaga na Simbodamalu umepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu ulipoanzishwa Oktoba 1 mwaka 2021 kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa serikali na wananchi wa eneo hilo.

Utoaji wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa shughuli za kuinua Ustawi wa Mtoto katika nyanja ya Elimu, Afya na Lishe, Maji, Usafi wa mazingira kupitia Mradi wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Lutende AP katika wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora.







Mwisho

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages