Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ametoa agizo kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutozifunga kampuni zinazodaiwa badala yake kukaa na Wafanyabiashara na kutatua changamoto walizonazo katika masuala ya Leseni na Usajili wa Makampuni ili kuboresha Mazingira ya Biashara.
Waziri Dkt. Kijaji ametoa agizo hilo leo Jumatano Oktoba 26, 2022 jijini Dodoma, wakati wa kikao cha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipopokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya BRELA.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutengeneza Mazingira ya Biashara kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara BLUEPRINT hivyo ameitaka BRELA kuendelea kutoa elimu ya Usajili wa Makampuni, Leseni na Umiliki Manufaa.
Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma za BRELA ikiwemo Uwasilishaji wa taarifa za wamiliki manufaa, uhusiano wa biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar na Sheria ya Leseni za Biashara na usajili wa viwanda ya mwaka 1967 ambayo inauhitaji mkubwa wa kuifanyia marekebisho.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile (Mb) ameipongeza BRELA kwa kazi nzuri na kusema kuwa ni wakati sasa wa Wizara kuzileta pamoja taasisi zake za BRELA, EPZA na TIC ambazo zinahusika na utoaji wa Leseni au vibali ili kuwa na takwimu sahihi za Wafanyabiashara Nchini nzima.
Akijibu baadhi ya maswali ya Wajumbe wa Kamati hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa ameahidi kuwa BRELA itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika utoaji wa huduma na kutumia mifumo ya Kielektroniki ya Utoaji Huduma za Sajili (ORS) na Utoaji wa Leseni za Biashara (NBP).
Awali akiwasilisha taarifa ya usajili wa Makampuni pamoja na jukumu la utoaji Leseni Kaimu Mkuu wa sehemu ya Makampuni BRELA Bi. Leticia Zavu amesema kuwa BRELA imekuwa ikitoa elimu ya mara kwa mara kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwa waliosajili kampuni, kampeni juu ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA na ukaguzi elimishi kwa kuwatembelea Wafanyabiashara kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.