Jumla ya Wanafunzi kumi wamethibitishwa kufariki, huku mmoja akiwa hajulikani aliko baada ya kutokea kwa ajali ya boti iliyoendeshwa kwenye Mto Mekong, katika jimbo la Kandal kusini mwa nchi ya Cambodia na wengine wanne kuokolewa.
Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Am Thou amesema ajali hiyo ya kusikitisha ilihusisha mashua ndogo iliyojaa kupita kiasi iliyokuwa inaelekea kusini mashariki mwa jimbo la Kandal, na kuongeza kuwa wengi wa Wanafunzi waliofariki walikuwa na umri kati ya miaka 12-15.
Amesema, ajali hiyo ilitokea Alhamisi jioni (Oktoba 13, 2022), majira ya saa 7:00 mchana, wakati mashua hiyo ikiwa imebeba watu 15, wakiwemo wafanyakazi wawili wa boti na wanafunzi 13 na ilizama takriban mita 50 kutoka ufukweni katika wilaya ya Leuk Daek.
Tayari Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Sen ametoa salamu za rambirambi na kuwataka watu kuwa waangalifu wakati huu wa mafuriko ambayo yameongeza ujazo wa Mto Mekong.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kandal, Chhoeun Sochet amesema, “Kufikia Ijumaa alasiri, miili 10 ilikuwa imepatikana, huku manusura wanne, wanafunzi wawili na wahudumu wawili wakiokolewa,na juhudi za uokoaji kwa aliyepotea bado zinaendelea.”
Ajali za boti, zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika taifa hilo la kusini mashariki mwa Asia ambapo mapema mwaka 2009, kivuko kilichojaa kupita kiasi kilipinduka kaskazini mashariki mwa Kambodia, na kuua abiria 17.
Source: Dar24