Breaking

Wednesday, 26 October 2022

USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA BURUNDI SEKTA YA MADINI WAANZA KAZI




Wizara ya Madini imepokea ugeni kutoka Jamhuri ya Burundi ikiwa ni matokeo ya kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi katika Sekta ya Madini.

Kufuatia kusainiwa kwa makubaliano hayo, ujumbe kutoka Burundi umekuja nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza namna bora ya kusimamia rasilimali madini.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na jiolojia ya Tanzania na jiolojia ya Burundi, uhusiano wa jiolojia ya Tanzania na jiolojia ya Burundi na majukumu ya wizara katika kusimamia Sekta ya Madini.

Aidha, ujumbe huo umefahamishwa kuhusu masuala ya uongezaji thamani madini, ushirikishwaji wa wazawa katika uchumi wa madini.

Pia, ujumbe huo, umepatiwa elimu kuhusiana na maandalizi ya Kufunga Migodi (Mining Closure), upatikanaji wa leseni pamoja na aina za leseni zinazotolewa nchini Tanzania.

Akiwasilisha mada Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewataka washiriki kujifunza kwa weledi mbinu bora za usimamizi wa Sekta ya Madini na kuuliza maswali yatakayo wasaidia kuboresha usimamizi wa sekta hiyo nchini kwao.

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi umeongozwa na Mshauri wa Rais katika Sekta ya Madini wa Burundi Alphonsia Kwizera ambao wamepata fursa ya kutembelea migodi mbalimbali ya wachimbaji wadogo mkoani Dodoma pamoja na mgodi wa kati wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Shanta Singida.

Tanzania na Burundi zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika usimamizi wa rasilimali madini baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan kufanya ziara nchini Burundi ambapo utekelezaji wake umeanza kufanyika kwa lengo la kuzinufaisha nchi hizo.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages