
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa leo Oktoba 20, 2022 amefungua Tamasha la pili la Kimataifa la Michezo kwa Wanawake la Tanzanite jijini Dar es Salaam na kutoa maelekezo mahususi ya kuendeleza michezo kwa Wanawake nchini.
Katika Tamasha hilo amewapongeza wanawake kwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kimataifa huku akitolea mfano wa timu ya Serengeti Girls kufuzu robo fainali Kombe la Dunia.
Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika ukombozi wa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.

Amewataka waandaji wa kuboresha Tamasha hili ambapo katika mwaka ujao liwe na mwakilishi kila wilaya.
Pia ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa ( BMT) kuimarisha Vyama na Mashirikisho ya Michezo katika kila wilaya ili kupata vipaji vingi.
Amesema watanzania wana vipaji vikubwa ambavyo havijaibuliwa na kufafanua kuwa kwa sasa tayari Wizara imeanzisha programu ya kusaka na kuibua vipaji ya Mtaa kwa Mtaa itakayokwenda nchi nzima kusaka vipaji hivyo.

Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuratibu mashindano ya Afrika ya Soka kwa Wanawake 2026 na AFCON Kwa mwaka 2027.
"Mimi naamini inawezekana tukiweka mikakati ya kujenga miundombinu, kudhibiti upendeleo, ukiritimba tunaweza kucheza kombe la Dunia lijalo mwaka 2030" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Aidha, ametoa wito katika Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kwamba hiyo itapunguza bajeti ya afya.
Amesema Tamasha hilo ni la pili baada ya lile la mwaka jana na kwamba kufanyika kwa mwaka hilo pia ni maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan yakutaka kuendelea kulifanya Tamasha hilo kila mwaka ili kutoa hamasa kwa Wanawake kote nchini kushiriki kwenye michezo na kujipatia ajira.
"Tumeendelea kutekeleza maono na maelekezo ya Mhe. Rais ambaye ana ndoto za kuona tunaibua vipaji vya Wanawake wa Tanzania kwenye michezo na kuviendeleza." Ameongeza Mhe. Mchengerwa

Waziri Mchengerwa amewaomba wanamichezo na watanzania kuja kushuhudia Tamasha hilo la siku tatu kuanzia leo ambalo litaleta burudani ya aina yake.
Tamasha hilo limeanza leo kwa kufanya kongamano kubwa na kujadili masuala mbalimbali ya michezo ikiwa ni pamoja na uongozi na utawala, mchango wa michezo katika ukuwaji wa kiuchumi na kijamii, udhamini wa michezo kwa Wanawake, vyombo vya Habari na Masoko.
Kesho michezo mbalimbali itachezwa ikiwa ni pamoja na mechi ya netiboli baina ya Tanzania na Uganda.
Michezo mingine itakayofanyika ni dondi, riadha, kareti, kabbadi, kikapu , nyavu, kunyanyua vitu vizito na Michezo ya jadi.
Katika Tamasha hili msanii Lina Sanga ametumiiza na kukonga nyoyo za washiriki.