KAMANDA wa Polisi mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)Bladius Chatanda amenusurika katika ajali ya gari baada ya gari lake binafsi kugongana uso kwa uso na gari binafsi la askari Polisi,F 5814 Koplo(CPL),Timoth Philipo wa Wilaya ya Busega ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa LEO na Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu kupitia kwa Kamishina Msaidizi wa polisi(ACP)Shadrack Masija kwa waandishi wa habari imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea Oktoba 2 mwaka huu majira ya saa 2:15 usiku katika Eneo la Nyakabidi mita chache kabla ya kufika eneo la mzani wa barabarani wa kupimia uzito magari.
ACP Masija akiongea kwa niaba ya Kamanda wa polisi mkoani humo amesema kuwa ajali hiyo imeyahusisha magari mawili yenye namba za usajili T462 BBD aina Toyota Harrier iliyokuwa ikiendeshwa na Blasius Chatanda na gari namba T 766 CCZ aina ya Toyota Mark II iliyokuwa ikiendeshwa na Timoth Philipo.
Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo kimetokana na dereva Timoth aliyekuwa akitokea mjini Bariadi kwenda Lamadi wilayani Busega kuhama ghafla upande wake wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia na kugongana uso kwa uso na gari aliyokuwa akiendesha Chatanda akitokea Lamadi kwenda Bariadi.
Kamanda Masija ameeleza kuwa katika gari la Chatanda alikuwa na msaidizi wake wa kazini,Askari Polisi H.7123 Polisi Konstebo(PC),Emanuel ambao wote watatu walijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Simiyu kwa ajili ya matibabu lakini Askari Polisi,Timoth alifariki dunia Oktoba 3 mwaka huu akiwa anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo huku wengine wakiendelea na matibabu na kwa sasa wameruhusiwa kwenda nyumbani.
Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu linatoa pole kwa familia ya Askari Polisi huyo aliyefariki dunia na litashirikiana na familia ya marehemu katika shughuli zote za mazishi ambayo yatafanyika wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza.
Akizungumza kwa njia ya Simu,Rpc Chatanda amesema ya kuwa anaendelea vizuri kwa sasa ameruhusiwa kutoka hospitali na yuko nyumbani akiwa amepumzika akiangalia hali yake kwani alipata maumivu sehemu mbalimbali za mwili.
Katika hatua nyingine,Mamia ya Wakazi wa Mji wa Maswa wamejitokeza leo kuaga mwili wa Koplo Timothy ambaye alifariki katika ajali hiyo ya gari.
Askari Polisi,Timothy kabla ya kuhamia wilaya ya Busega alifanya kazi wilaya ya Maswa hivyo familia yake ilikuwa ikiishi mjini Maswa maeneo ya Njiapanda ya Lalago.
MWISHO