WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugezi wa Kampuni binafsi ya JUMEME, Bi. Aida Kiyanga iliyepewa kazi ya kusambaza umeme katika visiwa vya Ukara na Irugwa wilayani Ukerewe mkoani Mwanza aripoti ofisini kwake jijini Dodoma Ijumaa hii (Oktoba 21, 2022) saa tano asubuhi ili akatoe maelezo kuhusu ucheleweshaji wa mradi huo.
Majaliwa amesema kuwa kampuni hiyo ilipewa na Serikali kazi ya kusambaza umeme kwenye kaya 289 katika visiwa vya Ukara na Irugwa wilayani humo lakini utendaji wake umekuwa wa kusuasua hali ambayo haiwezi kufumbiwa macho na viongozi wanaomsaidia kazi Rais Samia Suluhu Hassan kumaliza kero ya umeme kwa wananchi wa visiwa hivyo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Oktoba 17, 2022) wakati akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho ambako alikwenda kukagua ujenzi wa sekondari na kupokea taarifa ya ujenzi kituo cha afya Irugwa.
Pia ameagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo washiriki katika kikao hicho.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwahudumia wananchi kwa kutoa fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya. "Serikali imewapatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa kituo cha afya Irugwa."
Kuhusu ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa miradi mbalimbali inayogharimiwa na Serikali, Waziri Mkuu amewasihi watumie fursa hiyo kujipatia kipato kwa kufanya kazi zote wanazozimudu badala ya kuwaachi watu kutoka nje ya maeneo yao.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa madarasa hayo, Mheshimiwa Majaliwa amempongeza Mkuu wa Shule hiyo, Bi. Leocadia Vedastus na Diwani wa Kata hiyo, Bw. Sabato Joseph kwa usimamizi mzuri wa fedha zilizotumika katika ujenzi.
Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na matumizi mazuri ya shilingi milioni 120 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita katika shule ya Sekondari Irugwa wilayani Ukerewe. "Kila darasa hapa limejengwa kwa shilingi milioni 20 tena kwa viwango na ubora wa hali juu."
Mapema, akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa mwishoni mwa mwaka 2020 kwamba angerejea katika kisiwa hicho. "Kurejea kwako katika kisiwa hiki ni heshima kubwa kwa Wana-Irugwa na umepata fursa ya kuona shughuli za kimaendeleo katika kisiwa hiki ikiwemo ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo katika shule ya sekondari Irugwa."
Naye, Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia malipo ya miradi mbalimbali katika jimbo hilo zikiwemo sh. bilioni 2.8 za ujenzi wa barabara.
"Tunaomba Serikali itafute suluhisho la tatizo la umeme katika visiwa vidogo vya Ukerewe, kwa sasa vinategemea umeme wa jua ambao haupatikani wakati wote."
Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa madarasa hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Irugwa, Bi. Leocadia Vedastus walipatiwa sh. milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita ambapo shilingi milioni 119.23 zimetumika kujenga madarasa hayo, kutengeneza viti 300 na meza 300, kuweka mfumo wa kuvuna maji ya mvua na umeme wa jua. Pia zilitumika kujenga matundu matano ya vyoo na mabafu matano kwenye bweni la wasichana ambalo lilijengwa kwa nguvu za wananchi.
Alisema ujenzi wa madarasa hayo umesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani kutoka wanafunzi 60 hadi 45 kwa darasa moja. Faida nyingine ni kumwezesha mwalimu kumfikia mwanafunzi moja kwa moja.
Amesema mradi huo umewawezesha wananchi wa kisiwa cha Irugwa kujipatia kipato kwa kufanya kazi mbalimbali za ujenzi katika mradi huo na kulipwa pesa.