Breaking

Wednesday, 5 October 2022

WAZIRI MKUU AHAMASISHA UTALII NA UWEKEZAJI MKUTANO WA UNWTO - ARUSHA




Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje nchi waje kuwekeza katika maeneo yaliyohifadhiwa kutokana na Tanzania kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na vivutio bora duniani.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo jijini Arusha alipokua akifungua Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa Duniani (UNWTO), Kanda ya Afrika ambao umehudhuriwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali wanachama wa shiraka la utalii duniani kamisheni ya Afrika (UNWTO).


Aidha, amewakaribisha wageni mbalimbali waitembelee Tanzania kwa kuwa ina vivutio Bora vya asili na vya utamaduni zikiwemo hifadhi za Taifa Serengeti ambayo ni hifadhi bora Barani Afrika, Mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika, Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ina utajiri mkubwa wa historia ya chimbuko la mwanadamu dunia, Hifadhi ya Nyerere na Zanzibar ambayo ni maarufu duniani na inasifika kwa kuwa na fukwe bora zenye mchanga mweupe na zao la Karafuu.


"Natumia fursa hii kuwakaribisha washiriki wote hapa Tanzania kwenye ardhi ya Mlima Kilimanjaro ambao unaweza kuuona popote lakini ukitaka kuupanda ni lazima uje Tanzania, hifadhi yetu mashuhuri ya Serengeti, Bonde la Kihistoria la Ngorongoro na Visiwa vyenye marashi ya Karafuu vya Zanzibar" alisema Waziri Mkuu Majaliwa.


Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Mkutano wa 65 wa Utalii Kamisheni ya Afrika (UNWTO) utasaidia kuongeza chachu ya sekta ya utalii nchini na kuendeleza zao la utalii wa Mikutano yani (MICE TOURISM)


Ameongeza kuwa kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa 65 wa Utalii Kamisheni ya Afrika ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya nchi yetu na Jumuiya ya Kimataifa hususan katika Sekta ya Utalii.


"Kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano huu 65 ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya nchi yetu na Jumuiya ya Kimataifa hususan katika Sekta ya Utalii" Amesema Dkt. Chana.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages