Breaking

Wednesday 12 October 2022

WADAU WA MAENDELEO WAHIMIZWA KUCHANGIA MISAADA YA KIBINADAMU WAKATI WA MAAFA



Na Mwandishi wetu- Kilimanjaro

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewahimiza wadau wa maendeleo na watu binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuchangia vifaa vya misaada ya kibinadamu wakati wa maafa.

Mhe. Ummy aliyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua ghala la kuhifadhi vifaa vya misaada ya kibinadamu wakati wa maafa Kanda ya Kaskazini lililopo maeneo ya Chekereni, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Alisema uungwaji mkono wa serikali kutoka kwa wadau unasadia wananchi kufikiwa na huduma kwa haraka kutokana na majanga yaliyojitokeza ambayo husabababisha madhara kama vifo, ulemavu wa kudumu, mali kuharibika pamoja na miundombinu.

“Nitoe wito kwa wadau na watu mbalimbali ambao wanaguswa kushirikiana na serikali kwa kutoa vifaa wafanye hivyo pengine ngaji ya Wilaya, Mkoa na hata kijiji ili tuwe navyo vya kutosha ili yanapotokea tunatoa msaada kwa haraka,” alihimiza Mhe. Ummy.

Pia Mhe. Ummy alisisitiza utunzwaji wa magahala hayo hatua itakayosaidia vifaa hivyo kudumu kwa muda mrefu na kuwa tayari kutumika pindi vinapohitajika katika maeneo yenye maafa.

Aidha aliupongeza uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa utayari wa kutoa msaada wa kibinadamu kwa wananchi wanaokumbwa na maafa kwa lengo la kuwasaidia kurejea katika hali yao ya awali.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni Afisa Mifugo katika Mkoa huo Bwa. James Shao alisema ghala la Kanda ya Kasikazini linahudumia Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

MWISHO
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages