MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku 14 kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwasilisha majibu yake dhidi ya kesi ya madai aliyofunguliwa na mfanyabiashara Patrick Kamwelwe ya kupora Range Rover.
Amri hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi ilipotajwa kwa mara ya kwanza.
Hakimu Kabate alitoa amri hiyo baada ya Wakili Gift Joshua anayemwakilisha Paul Makonda ambaye ni mdaiwa wa pili katika kesi hiyo Na. 234/2022, kudai kuwa mteja wake hajapata hati ya madai.
Kufuatia madai hayo, Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 8 Novemba 2022, ambapo itatajwa tena.
Kamwelwe amefungua kesi hiyo ya madai, akiiomba mahakama imuamuru Makonda na mwenzake, William Malecela maarufu kama Le Mutuz, wamlipe zaidi ya Sh. 247.2 milioni, kama fidia ya kupora gari lake aina ya Range Rover.
Kamwelwe anadai kuwa Makonda kupitia kwa Le Mutuz, alimuazima gari hilo kwa ajili ya kulitumia kwa muda wa wiki mbili, kisha alirudishe lakini hadi sasa hajarudishiwa gari lake.
Katika kesi hiyo, Kamwelwe anaiomba mahakama imuamuru Makonda na mwenzake, kumlipa kiasi hicho cha fedha kama fidia anayodai kuwa, imetokana na hatua ya wadaiwa hao kumdhulumu gari lake jeusi aina ya Toyota Land Rover/Range Rover Sport, yenye namba za chesis 20153.
Source: Global Publishers