Mwanahamisi Msangi na Tito Mselem, Morogoro
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema kuwepo kwa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge mkoani Morogoro kutaleta manufaa mapana kwa wachimbaji wa madini, wafanyabiashara wa madini na wananchi wa wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2022 mkoani Morogoro wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge ambapo Ofisi hiyo itahudumia Wilaya tatu za Ulanga, Malinyi na Kilombero na kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi.
Dkt. Biteko ameendelea kusema Ofisi hiyo italeta tija kwa jamii inayozunguka migodi kwani itaweza kusimamia na kuratibu kwa karibu utekelezaji wa wajibu wa migodi kwa jamii (CSR) pamoja na kushirikisha wazawa katika kutoa huduma na ajira (Local Content).
“Katika kipindi hiki ambacho migodi ya uchimbaji wa kati na mkubwa wa madini ya Kinywe inategemea kuanza uzalishaji na kutoa ajira kwa wazawa itasaidia kuinua uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Pia, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wachimbaji ,watafiti, wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kuwa kila gramu, karati na Tani za madini zipelekwe sokoni ili serikali ipate fedha na kuachana na utoroshaji.
Vilevile, Dkt. Biteko amemuelekeza Afisa Madini Mkazi Mahenge Jonas Mwano kutembelea maeneo yote ya wachimbaji na kutoa elimu juu ya ada, aina ya madini na bei elekezi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa ameshukuru kwa kuipandisha hadhi wilaya ya Ulanga kwa kuanzisha Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge itakayorahisisha utoaji huduma kwa wananchi.
Ametoa wito kwa Wafanyabishara wa madini kufuata Sheria bila shuruti na kumuhakikishia Dkt. Biteko kusimamia makusanyo pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini katika wilaya yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Danstan Kitandula amemshukuru Waziri wa Madini kwa kuona umuhimu wa kuialika Kamati hiyo katika ufunguzi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge ambapo uwekezaji utafanyika kwa tija.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolf Ndunguru amesema Morogoro ni mkoa wa kipekee na umejaaliwa kuwa na madini ya kimkakati ya Kinywe na kwamba ufunguzi wa ofisi hiyo ni fursa ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi ya kuiwezesha Sekta hii kuchangia asilimia 10 katika pato la taifa ifikapo 2025.
Naye, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema mkoa wa kimadini wa Mahenge unaohusisha Wilaya tatu, Ulanga, Malinyi na Kilombero ambapo utasimamia jumla ya leseni za wafanyabishara wakubwa wa madini (dealers) 62 , wafanyabiashara wadogo wa madini (Brokers) 68 , uchimbaji mdogo 277, leseni ya uchimbaji mkubwa moja (1) ya kampuni ya Faru Graphite, leseni 3 za uchimbaji wa kati leseni za utafiti 18.
Pia, amesema kuna leseni za utafiti 18 lengo ni kuhakikisha kwamba utafiti unafanyika na migodi ya kati inafunguliwa katika wilaya hizo ili kuhakikisha uchumi wa maeneo hayo yanaimarika kwa manufaa ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.