Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 34, huenda atakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua katika kaunti ya Nyeri Nchini Kenya baada ya kudaiwa kupatikana akijaribu kumtupa mpwa wake mwenye ugonjwa wa kupooza ubongo msituni.
Mshukiwa, Lydia Wanjugu anadaiwa kupanga mpango huo na dada yake wa kumtupa mtoto huo mwenye umri wa miaka 13 msituni.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, Wanjugu anaripotiwa kuonekana akiwa amebeba gunia nzito na kuingia msituni jambo ambalo liliwachochea umma kumfuata.
Ndipo wakazi waligundua kwamba alikuwa amembeba mtoto huyo baada ya kula njama na dada yake kumuua.
Kisha alikamatwa na wanachama wa Nyumba Kumi ambao walimbeba juu kwa juu hadi katika Kituo cha Polisi cha Narumoru.
“Wanjugu alifikishwa polisi na wanachama wa Nyumba Kumi baada ya kumkamata wakati akijaribu kumchukua mtoto wa miaka 13 anayesumbuliwa na ugonjwa wa mtindio wa ubongo na kumpeleka kwenye msitu huo ili afie huko. Mwathiriwa alikuwa mtoto wa dada yake. Alionekana na umma akiwa amebeba gunia zito akiingia msituni na wakamfuata,” ilisoma ripoti ya polisi.
Mtoto huyo alipelekwa katika katika kituo cha Metropolitan Sanctuary ambako watoto wenye ulemavu hutunzwa.