Na.Samwel Mtuwa- Geita.
Naibu Katibu Mkuu Uwekezaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara Ally Gugu ameipongeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kuendelea kuibua vyanzo vipya vya uwekezaji katika Sekta ya Madini kupitia tafiti zinazofanywa na GST ambazo zinazotoa taarifa za uwepo wa Madini katika maeneo mbalimbali.
Hayo amesema Leo Oktoba 4, 2022 alipotembelea banda la GST katika Maonesho ya Tano ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.
Kiuhalisia Sekta ya Madini ni sekta mtambuka hivyo jinsi mnavyofanya tafiti zenu mnaongeza wigo wa kupata uwekezaji kupitia taarifa zenu ambazo zinatoa picha juu ya uwepo wa Madini katika eneo husika.
Akiuliza juu ya GST inavyowasaidia wachimbaji wadogo wa Madini , Mkutubi Mwandamizi kutoka GST Ernest Luhoko alimweleza kuwa GST inawasaidia wachimbaji wadogo kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwafanyia tafiti katika maeneo yao ili kubaini mwelekeo wa mbale inayobeba madini na namna bora ya kuchenjua madini yao.
Aidha, hivi karibuni GST imetoa mwongozo ambao umetoa elimu kwa wachimbaji wadogo juu ya namna bora ya uchukuaji wa sampuli za miamba na madini kwa ajili ya uchunguzi na uchenjuaji Katika Maabara ya madini ili kupata sampuli wakilishi ambayo itatoa majibu sahihi yanayowakilisha miamba na madini yanayopatikana katika maeneo yao na hivyo kuwaongezea tija katika kazi zao.
Baada ya kupokea taarifa hizo Naibu Katibu Mkuu Uwekezaji aliwashukuru wataalam wa GST Kwa Maelezo mazuri.