Wananchi wengi kutoka katika mkoa wa Pwani na mikoa ya jirani wameomba elimu kuhusu madini kujumuishwa kwenye mitaala ya shule za msingi na sekondari na kuhamasisha wanafunzi wengi kujiunga zaidi kwa shahada ya jiolojia katika vyuo vikuu nchini na kuongeza wataalam kwenye Sekta ya Madini.
Waliyazungumza hayo kwenye kilele cha Maonesho ya Tatu ya Uwekezaji na Biashara yaliyofanyika katika Viwanja vya SIDO, Maili Moja Mkoani Pwani Oktoba 10, 2022 ambayo yalilenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa wa Pwani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao waliomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutengeneza mitaala ya elimu ya madini kama mkakati mmoja wapo wa kukuza waalam wa madini nchini.