Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Omary Kipanga amesema kuwa kufikia mwezi Disemba mwaka huu 2022 wizara ya elimu itazindua sera mpya ya elimu ili kuleta mabadiliko ya kielimu nchini.
Ni katika uzinduzi wa kongamano la saba la kimataifa la uhandisi mitambo na viwanda uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Oktoba 20, Naibu Waziri wa Elimu Omary Juma Kipanga anaweka bayana kuwa ili kuwa na wahitimu wenye maatifa zaidi wizara yake imeanza kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa wizara hiyo Aprili 22, 2021, Bungeni Dodoma ya kutaka ifanye mabadiliko ya sera, mitaala na sheria ya elimu.
"Katika sheria na sera hii ijayo, elimu ya msingi itaishia darasa la 6 na hakutakuwa na mtihani wa Taifa bali tutakuwa na course assessment, baada ya kufaulu mwanafunzi atajiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo atakuwa tayari na mchepuo rasmi, kama ni kilimo ni kilimo, hakuna kusoma vitu vyote na tutakuwa na michepuo karibu 15 hivi, tunalenga huyu kijana akihitimu kidato cha 4 awe na uwezo wa kuwa na maarifa fulani na ujuzi ili aajirike au aajiriwe kama hatakwenda kidato cha 5," amesema Naibu Waziri Kipanga
Aidha Naibu Waziri Kipanga ameongeza, "Kuna mtazamo ambao mimi ninasema kwamba ndio uhalisia, wahitimu wengi hawaajiriki na hawana maarifa ya kujiajiri, hii ni changamoto sasa, sisi kama Wizara husika, tulipokea maelekezo ya Rais Samia alipohutubia Bunge Aprili 22, 2021, alitutaka tufanye mabadiliko ya sera, sheria na mitaala ya elimu yetu, sasa kufikia mwezi Desemba mwaka huu lazima tutazindua sera mpya ya elimu kwa lengo la kuleta mabadiliko kwenye mfumo wa elimu yetu na wataalam wetu na hapa tutaanza na elimu ya msingi hadi vyuo vikuu".
Via EATV