Breaking

Friday, 7 October 2022

WANANCHI MSITISHWE UTEKELEZAJI BIMA YA AFYA KWA WOTE- PROF. MAKUBI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imewaomba wananchi kuunga mkono suala la Bima ya Afya kwa Wote na kupuuza vitisho juu ya suala hilo kwa kuwa ndilo mkombozi wa Afya za Watanzania.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi wakati akifungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

"Wananchi wasitishwe na wala usiogope juu ya sheria hii, tunahitaji kila Mtanzania awe na bima ya Afya na hata kwa wananchi wasio na uwezo, Serikali imeweka mazingira ya kuwatambua na kuwapa kadi maalum za kupata huduma za matibabu hivyo tuunge mkono suala hili ambalo ndio mkombozi mkubwa katika Afya zetu," alisema Prof. Makubi.

Akizungumzia madhumuni ya kutungwa kwa sheria hii, alisema ni kutokana na kuwepo kwa upungufu wa kisheria katika Mfumo wa Bima ya Afya uliosababisha idadi kubwa ya wananchi kutokuwa na bima ya Afya hivyo kukosa uhakika wa kupata huduma za matibabu.

Alisema kuwepo kwa sheria hii ya Bima ya Afya kwa Wote kutawezesha wananchi wengi kuwa katika Mfumo wa bima ya Afya hivyo kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wanapozihitaji.

"Ili kila mwananchi aweze kushiriki shughuli za maendeleo ni lazima awe na uhakika wa Afya yake kupitia uhakika wa kupata matibabu lakini sheria hii itasaidia kuwaepusha wananchi kuingia kwenye janga la umasikini ambalo hutokana na gharama kubwa za matibabu hivyo jambo hili ni muhimu na tulipe kipaumbele," alisisitiza Prof. Makubi.

Alieleza kuwa Sheria hii inakwenda kuweka usawa katika kitita cha mafao kwa wananchi watakaojiunga na bima ya Afya lakini kuwa na fursa ya wananchi wote kupata huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma vya umma na binafsi kuanzia ngazi ya Zahanati hadi ngazi ya Taifa.

Akizungumzia uchangiaji, alisema kuwa sheria itaweka viwango vya michango kulingana na hali halisi ya gharama za utoaji wa huduma za Afya ambapo viwango pendekezwa kwa sasa ni Shilingi 340,000 kwa kaya ya watu sita.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha huduma zitakazotolewa zinakuwa bora zaidi.

"Naagiza vituo vyote vijipange kutoa huduma bora kwani Serikali tayari imeshaweka mazingira mazuri kwa kuweka vifaa tiba vya kisasa na upatikanaji wa dawa kwa sasa ni mkubwa," alisema Prof. Makubi.

Akizungumzia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, alisema Mfuko umefanya kazi kubwa na nzuri ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha huduma za matibabu nchini.

Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Edward Mbanga akitoa maelezo ya awali, alisema kuwa Sera ya Afya inataka mwananchi kuchangia huduma za matibabu hivyo ujio wa Bima ya Afya kwa wote ni Mfumo imara unaomuwezesha mwananchi kupata huduma za matibabu wakati wowote.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages