Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2022 ambacho ni robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022-2023, Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 178.01 kwenye madini.
Mhandisi Samamba aliyasema hayo jana tarehe 28 Oktoba, 2022 kwenye Kikao cha 16 cha Tume ya Madini kilichofanyika Jijini Dodoma kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022-2023.
Aliongeza kuwa ili kuvuka lengo lililowekwa na Serikali la kukusanya shilingi bilioni 822 katika mwaka wa fedha 2022-2023, Tume ya Madini imeendelea kuidhinisha na kutoa leseni za madini kwa wakati kwa waombaji wenye sifa na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.
Aidha, alisema kuwa Tume imeendelea kusogeza huduma karibu na wadau wa madini kupitia uanzishwaji wa ofisi mpya za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, masoko na vituo vya ununuzi wa madini.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula sambamba na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na watendaji wa Tume, aliwataka watumishi wake kuongeza weledi, juhudi, ubunifu na uaminifu katika utendaji kazi.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa leseni za madini kuziendeleza ili Serikali iendelee kunufaika na rasilimali zake.
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo akizungumza katika kikao hicho, alisema kuwa, katika kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini, Tume ya Madini imeendelea kuhakiki mipango ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini (local content) pamoja na kutoa elimu kwa Kampuni za uchimbaji na utoaji huduma.
"Mafanikio makubwa sana yameonekana katika eneo hili kwa kuwa kumekuwepo na mwamko mkubwa sana kwa wananchi wanaozunguka migodi kutokana na matokeo ya elimu ambayo imekuwa inatolewa na Tume ya Madini kuhusu namna wanavyoweza kushiriki kwenye fursa za uwekezaji zilizopo kama vile utoaji wa huduma mbalimbali na ajira," alisisitiza Lekashingo.
Kikao hicho cha siku moja kilishirikisha Makamishna wa Tume ya Madini ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Dkt. Faraji Mnyepe, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa na mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Seushi Mburi.
Makamishna wengine ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Haroun Kinega, Profesa Abdulkarim Mruma, Janet Lekashingo na Menejimenti ya Tume ya Madini.