Breaking

Friday, 30 September 2022

WIZARA YA MAJI, NISHATI NA MADINI ZANZIBAR YATEMBELEA BANDA LA TUME YA MADINI, TGC KWENYE MAONESHO YA MADINI GEITA




Timu ya wataalam ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini, Mhandisi Said Mdungi kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar imetembelea banda la Tume ya Madini na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwenye Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Bombambili, mjini Geita.

Mara baada ya kupata elimu kuhusu madini mbalimbali yanayopatikana nchini pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya Madini wameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa usimamizi mzuri wa sekta ya madini na kuongeza kuwa wataendelea kufanya ziara mbalimbali nchini kwa ajili ya kujifunza siri ya usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini.




Akizungumza kwenye mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini Zanzibar, Mhandisi Said Mdungi amesema kuwa lengo la kutembelea maonesho hayo, ni kujifunza namna shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini sambamba na fursa nyingine muhimu zilizopo nchini ili kupata uzoefu na kuboresha utendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Sekta ya Madini.

“Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha muungano, tutaendelea kushirikiana kupitia Sekta ya Madini kwa kubadilishana uzoefu ili tupige hatua na kuvutia wawekezaji wengi zaidi nchini Zanzibar,” amesema Mhandisi Mdungi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages