Imeelezwa kuwa, tangu kufanyika kwa maboresho kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, zaidi ya shilingi bilioni 33.5 zimetumika katika miradi mbalimbali iliyotekelezwa na wamiliki wa leseni za miradi katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mafanikio na changamoto za utoaji na upatikanaji wa huduma kwa jamii kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.
Amesema Sheria ya Madini, Sura 123 ilivyofanyiwa maboresho na kuwekewa kifungu cha 105 ambacho kinaelezea utaratibu mzima wa kuandaa na kutekeleza mipango ya wajibu wa Kampuni kwa jamii, suala ambalo limekuwa na mafanikio makubwa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo kampuni zilikuwa zikiwajibika kwa jamii kwa utaratibu wanaojiamulia.
ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123, Mmiliki wa Leseni ya Madini analazimika kila mwaka kuandaa Mpango unaoaminika ambao umekubaliwa kwa pamoja na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kushauriana na Waziri anaye husika na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Waziri anaye husika na masuala ya Fedha ambapo mpango huo utaangazia masuala ya mazingira, kijamii, utamaduni na kiuchumi kwa kutoa kipaumbele kwa jamii inayozunguka mgodi.
Pamoja na mafanikio hayo, Samamba amesema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo juu ya wajibu wa kampuni kwa jamii na pia kumekuwepo na utekelezaji hafifu wa miradi kwa baadhi ya Halmashauri.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini Godfrey Nyamsenda amesema wizara imekamilisha Rasmi ya Kanuni zitakazo simamia masuala ya Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii ili kuboresha na kuweka usawa kwenye matokeo ya utekelezaji wa miradi.
Nyamsenda amesema uandaaji wa Rasimu ya hKanuni hiyo umezingatia matakwa ya Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo yanaeleza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa jamii katika miradi ya madini na kuhimiza kampuni za madini kuongeza uwajibikaji kwa jamii.
"Kanuni hizi ni muhimu kwa kuwa zinalenga kuondoa mapungufu yaliyokuwepo katika utekelezaji kwenye eneo la wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii kwa watekelezaji ikiwa ni sehemu ya matakwa ya Sheria ya Madini, Sura 123," amesema Nyamsenda.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema, wizara yake imeona ni sahihi kuwasilisha Rasimu ya Kanuni hiyo ili kupata maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo inasimamia Sekta hiyo.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolf Ndunguru ametoa ufafanuzi juu ya Rasimu hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maoni na ushauri uliyotolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo.