Breaking

Monday, 26 September 2022

WANAFUNZI WATATU WAFARIKI BAADA YA KUZAMA MTONI WAKITAFUTA MAJI YA KUFUA




Wanafunzi watatu wa shule ya msingi wamekufa maji katika Mto wa Kathita, kaunti ya Tharaka Nithi Nchini Kenya.

Watatu hao wenye umri wa miaka ya 13, 12 na 10 kutoka kwa Shule ya Msingi ya Gakuyu walikuwa wametembea kilomita kadhaa kutoka Kirikuma hadi kata ndogo ya Gituma wakitafuta maji ya kufua sare zao za shule wakati waliangamia Jumamosi, Septemba 24.

Chifu wa Gituma, Kibaara Muthungu, alisema watoto hao mmoja akiwa mtahiniwa wa darasa la nane walikuwa wakijaribu kuvuka mto hadi mahali ambapo wangeweza kufua sare zao wakati walipozama.

Wanafunzi kutoka eneo jirani la Kirukuma walikuja kuosha sare za shule na mifuko yao wakati walipozama," alisema Muthungu kama alivyonukuliwa na Shirika la habari la Nation.

Muthungu aliongeza kuwa mvulana mmoja ambaye alinusurika kifo kwa tundu la sindano ndiye alipiga kamsa na kuwavutia majirani ambao walikimbia katika eneo la tukio lakini tayari watatu hao walikuwa wamepoteza maisha yao Miili ya watatu hao ilichukuliwa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Marimanti Level Four.

Chifu msaidizi wa Gituma Josphat Muriungi alisema watoto wawili kati ya waliofariki walikuwa ndugu. Alisema kutokana na ukame unaoendelea kukumba kaunti hiyo na kusababisha kukauka kwa mito mingi inayotiririsha maji mwaka mzima, wakazi wanasafiri mbali kutafuta maji, kufua nguo na kunywesha mifugo yao katika Mto Kathita au Mto Tana.

Aliongeza kuwa wakazi wa maeneo mengi ya eneo bunge la Tharaka wanateseka kutokana na ukosefu wa maji na baa la njaa hivyo akaiomba serikali kuwapatia maji ya bomba kama suluhu ya kudumu.

Kulingana na Muriungi shule pia zinatarajiwa kuathirika kutokana na uhaba wa maji na kuitaka serikali ya kaunti kutafuta suluhu la haraka.

"Mito kadhaa ya kudumu na ya msimu hupitia eneo letu ikiwa ni pamoja na Mto Tana lakini watu bado wanateseka kwa ukosefu wa maji isipokuwa wale walio karibu na mito ambao pia wako katika hatari ya kuzama au hata kushambuliwa na mamba au viboko," alisema Muriungi.

Takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 38,517 katika sehemu zenye ukame za eneo bunge la Tharaka wanahitaji msaada wa chakula na maji.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages