Breaking

Thursday, 22 September 2022

TANZANIA KUPOKEA BILIONI 34 KUTOKA VODAFONE KUIMARISHA KUIMARISHA USAFIRI WA DHARURA KWA WAJAWAZITO



Na.WAF, New York, Marekani

Tanzania itapokea msaada wa Dola Milioni 15 (taribani shilingi Bilioni 34) kutoka Kampuni ya Vodafone ili kuwezesha usafiri wa dharura kwa wajawazito.

Ahadi hiyo imetolewa katika kikao cha pembezoni cha Mkutano Mkuu wa 77 wa Wakuu wa Nchi (UNGA) unaoendelea Jijini New York, Marekani.

Katika kikao hicho, chini ya Uenyekiti wa Mtendaji Mkuu wa Shirika la misaada la Marekani (USAID), Bibi Samantha Power, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa kampuni ya Vodafone Bw. Joachim Reiter aliwasilisha ahadi ya kampuni hiyo kutoa fedha hizo ili kutekeleza mradi huo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi nchini.

Alieleza kuwa makampuni binafsi yana jukumu muhimu la kushirikiana na serikali kuleta maendeleo na kuchangia ustawi wa jamii.

Serikali ya Marekani kupitia USAID huzipatia pia kampuni binafsi fedha kuwezesha kufikia nchi zenye uhitaji mkubwa.

Akimwakilisha Rais Samia katika mkutano huo, Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, aliishukuru Vodafone.


Dkt. Mpango alieleza kuwa nchini Tanzania takribani wanawake 4,000 na watoto 65,000 hufariki kila mwaka huku kuchelewa kupata huduma za dharura ikiwa ni pamoja na usafiri wa dharura kukichangia sehemu ya vifo hivyo .

Naye, Waziri wa Afya Ummy mwalimu aliyeambatana na Makamu wa Rais katika mkutano huo, alieleza furaha yake kwa Tanzania kupatiwa mradi huo.

Alisema mradi huo utaisaidia Tanzania kufikia malengo iliyojiwekea katika Mkakati wa Tano wa Afya na Mpango Mkakati wa Tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (one plan 3) ambayo moja ya vipaumbele ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto na hivyo ni chachu ya kuiwezesha nchi kufikia malengo endelevu ya kidunia.

MWISHO
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages