Breaking

Wednesday, 14 September 2022

WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA UKAMILISHAJI WA STENDI NYEGEZI, SOKO KUU MWANZA



OR -TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhe. Adam Malima kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Ujenzi wa Stendi ya Nyegezi na Soko Kuu la Mwanza Mjini inayoendelea kujengwa ili ikamilika kwa wakati.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo Septemba 14, 2022 wakati akitoa salamu za Wizara katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji na Kituo cha Kutibu Maji cha Butimba uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Bashungwa amesema, Serikali imeelekeza fedha nyingi za miradi katika Mkoa wa Mwanza na imeweka mikakati ya kuliwezesha jiji hilo liwe la kisasa na kimkakati kupitia miradi ya kupendezesha miji (Tactic).

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkuu wa Mkoa huyo kuimarisha usafi wa Jiji la Mwanza ikiwa ni pamoja na usafi katika Mto Mirongo ili Serikali inapoleta Sh bilioni 9.2 za kukarabati kingo za huo wenye urefu wa kilometa 9.5 zikute mto ukiwa safi.

Amesema mkakati wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikishirikiana na Ofisi ya Makamu Wa Rais (Muungano na Mazingira) ni kusimamia mikoa yote kuwa na programu ya maalum za kupanda miti na kuweka mipango endelevu ya kuimarisha usafi katika mikoa yote nchini.

Vile vile,Bashungwa amesema utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Chanzo cha Maji na Kituo cha Kutiba Maji cha Butimba utaleta mabadiliko makubwa kwa wananchi Mkoa Mwanza kwa kuwawezesha kupata huduma ya maji safi na salama ya kutosha.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages