Breaking

Monday, 19 September 2022

PANYA ROAD 135 WAKAMATWA DAR, MSAKO KUFANYWA VIJIWENI, VIBANDA UMIZA




Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amesema kwa siku nne tangu kuanza kwa operesheni ya kukabiliana na Panya Road Mkoa wa Dar es salaam upo salama baada ya kufanikiwa kuwakamata Watuhumiwa 135 na vifaa mbalimbali vilivyoibwa.

RC Makalla ameeleza hayo wakati wa kikao kazi cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kilichofanyika leo Jumatatu September 19, 2022 kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali ya usalama ya Mkoa pamoja na kupokea taarifa ya mwenendo wa operesheni ya kukamata Wahalifu.

Amesema kuwa wengi waliokamatwa vijana wenye umri kati ya miaka 14 na 30 waliobainika kuhusika na matukio ya uvamizi mitaani maarufu kama Panya Road na baada ya kuhojiwa ilibainika viongozi wa magenge hayo baadhi yao waliwahi kutumikia vifungo mbalimbali magerezani.

Ameeleza kuwa Mkoa umejipanga kuhakikisha matukio hayo hayajirudii huku akiitaja mipango ya kudhibiti uhalifu ikiwemo Vituo vyote vya Polisi kufanya kazi kwa saa 24, ongeze la doria kila Kata na kila Mtaa kufanya mkutano maalumu kujadili ajenda ya ulinzi na usalama kila Wiki ya kwanza ya Mwezi.

Mipango mingine ni msako kwa Wafanyabiashara wanaouza na kununua vifaa vya wizi, Kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi, ufuatiliaji wa mienendo ya Wafungwa waliomaliza kutumikia vifungo na msako kwenye vijiwe, majumba mabovu yasiyokamilika (mapagala) na vibanda umiza ambavyo vimekuwa sehemu ya kukutana na kuweka mipango.

Aidha ametoa wito kwa Wazazi kuhakikisha wanazingatia suala la malezi kwa kufuatilia mienendo ya Watoto wao.

Operesheni ya kukamata Panya Road ilizinduliwa September 15 na ndani ya siku nne imekuwa na mafanikio makubwa yaliyopelekea kukamatwa kwa Watuhumiwa 135, Wanunuzi watano wa vifaa vya wizi na kupatikana kwa mali zilizoibwa ikiwemo TV, Radio, simu za mkononi na vitu vingine.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages