Na Lucas Raphael,Tabora
HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 685.5 kwa vikundi 129 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022.
Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugezi Mtendaji wa Manispaa hiyo Dkt Peter Nyanja alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za maendeleo katika kikao cha baraza la madiwani.
Alifafanua kuwa kati ya vikundi hivyo 98 ni vya wanawake, 16 vya vijana na 15 vya watu wenye ulemavu ambapo wanawake walikopeshwa sh mil 536, vijana mil 126 na watu wenye ulemavu mil 23.5.
Alibainisha kuwa usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa mikopo hiyo umewezesha jumla ya sh mil 447.5 kurejeshwa ambapo vikundi vya wanawake vimerejesha jumla ya sh mil 351.2, vijana sh mil 69.3 na watu wenye ulemavu sh mil 26.9.
Aidha aliongeza kuwa kurejeshwa kwa mikopo hiyo kulitoa fursa kwa vikundi vingine kuwezeshwa ambapo sh mil 341zilizorejeshwa zilikopeshwa kwa vikundi vipya 70 ambavyo awali havikunufaika.
Dkt Nyanja alieleza kuwa ili kuhakikisha mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani inawanufaisha wajasiriamali wote, halmashauri imeweka utaratibu wa kuwapa fursa za kushiriki katika maonesho ya kibiashara ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao.
Alisema hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu jumla ya wajasiriamali 72 wamewezeshwa kushiriki maonesho ya Kitaifa na Kimataifa, yaliyoandaliwa na taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Maonesho ya East Africa (Juakali) na Maonesho ya Sabasaba ya jijini DSM.
Aidha jumla ya vikundi 95 vyenye wanachama 2,322 wanawake wakiwa 2,197 na wanaume 125 vinavyojihusisha na utoaji wa huduma za kifedha vimesajiliwa na kutambuliwa na vinaendelea kutekeleza shughuli zao kama kawaida.
Mstahiki Meya wa manispaa hiyo Ramadhan Kapela alisema katika kipindi cha mwaka 1 wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, jamii imenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia uwezeshwaji wa asilimia 10 za mapato ya ndani.
Alitaja baadhi ya mafanikio waliyopata kuwa ni kuundwa kwa vikundi vipya 240 huku 193 vikiwa vimekamilisha taratibu zote na kusajiliwa, kutoa kiasi kikubwa cha mikopo kwa vikundi vyote na kufanikiwa kukusanya sh mil 448 za mikopo hiyo sawa na asilimia 70 ya mikopo hiyo.
Mwisho.