Breaking

Wednesday, 21 September 2022

SERIKALI YATATUA MGOGORO WA MPAKA KATIKA HIFADHI YA MSITU MPANDA NORTH EAST




Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetatua mgogoro kati ya Hifadhi ya Mpanda North East na wananchi wa Kijiji cha Vikonge Mkoani Katavi kuhusu mipaka ya eneo hilo.

Hayo yamesemwa Septemba 21,2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Mhe. Selemani Kakoso kuhusu Serikali kumaliza mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Vikonge na Nomalusambo dhidi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

“Wizara kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji, wananchi pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitafsiri mipaka ya eneo hilo ili kutatua mgogoro wa mpaka” Mhe. Masanja amesisitiza.

Aidha, amewataka wananchi kuheshimu makubaliano yaliyosainiwa kati ya Kijiji cha Vikonge na TFS juu ya mpaka.

Akizungumzia kuhusu Kijiji cha Nomalusambo ambacho kina Kitongoji cha Ijenje kilichopo ndani ya Hifadhi ya Mpanda North East, Mhe. Masanja amesema mwaka 2017 kitongoji hicho kiliondolewa katika eneo la hifadhi wakati wa zoezi la uondoaji wavamizi msituni ambapo wananchi walitii maelekezo na kuondoka ndani ya hifadhi.

Mhe. Masanja amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages