Asteria Muhozya na Steven Nyamiti- Dodoma
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa tayari imekwisha kuchukua hatua kadhaa za kushughulikia changamoto ya uwepo wa tozo nyingi zinazotozwa na Taasisi nyingine za Serikali kwa wachimbaji wadogo wa madini ikilenga kuwezesha shughuli hizo kufanyika kwa tija.
Mhandisi Samamba ameyasema hayo katika warsha ya Siku moja kwa kamati hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa lengo la kuijengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya madini ikiwemo mwenendo wa sekta na biashara ya madini nchini.
Amesema kuwa, tayari Wizara imekwisha kutana na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana kuhusu utitiri wa tozo kwa wachimbaji wadogo wa madini zinazotozwa na taasisi nyingine suala ambalo linapelekea kuwepo changamoto kwenye utekelezaji wa shughuli na biashara ya madini.
Pia, ameeleza kuwa, tayari Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022, imefanya mabadiliko kwenye Sheria ya TASAC na kuongeza kwamba, Tume ya Madini inatarajia kukutana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kujadiliana kuhusu suala la tozo kwa wachimbaji wadogo ikiwemo kukutana na Wakurugenzi wa Halmashauri na wadau wa madini kwa ajili ya ufumbuzi na kutatua changamoto hiyo katika kikao kinachotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Akizungumzia mwenendo wa hali ya uwekezaji katika Sekta amesema, uwekezaji umeendelea kuongezeka kutokana na juhudi zinazofanywa na wizara za kuvutia uwekezaji na kueleza kwamba, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23 Tume ya Madini imepanga kutoa Leseni 9,172.
Pia, ameileza kamati hiyo kuwa, baada ya kanzishwa kwake mwaka 2017, ilipewa majukumu 22, huku majukumu matatu makuu yakiwa ni ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi na utoaji wa leseni, ukaguzi wa migodi na udhibiti wa biashara ya madini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse akieleza hali ya uwekezaji kwa shirika hilo pamoja na mambo mengine ameeleza kwamba, kwa mara ya kwanza shirika hilo linatarajia kuanzisha mgodi wake mwenyewe katika leseni ya dhahabu ya Kigosi mkoani Geita na tayari fedha za utekelezaji huo zimetengwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 ambapo linatarajia kukamilisha utafiti kwa ajili ya maandalizi ya uchimbaji dhahabu.
Akizungumzia mipango ya shirika hilo amesema ni pamoja na kuongeza mapato yake ya ndani kwa mwaka huu wa fedha ambapo linatarajia mapato hayo kufikia shilingi bilioni 70 na kuondokana kabisa utegemezi wa fedha za serikali.
Dkt. Mwasse ameeleza mipango mingine na kuitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za uchorongaji kwa kununua mitambo na vifaa vya kisasa zaidi sambamba na kutafuta kandarasi zaidi za uchorongaji katika migodi mikubwa ya kati ndani na nje ya nchi.
Pia, ameongeza kuwa shirika hilo limepanga kuimarisha miradi yake ya uchimbaji wa makaa ya mawe na kuongeza mitambo ya utengenezaji wa Mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) utaosambazwa maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewasilisha kwa kamati hiyo Mfumo wa kudhibiti biashara ya Tanzanite ikiwa pia ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu aliyoyatoa mwaka 2021, wakati akizindua Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery ambapo Rais Samia aliitaka wizara kuongeza thamani ya madini hayo ikiwemo kuhakikisha yanalinufaisha taifa kutokana na upekee wake.
Wakitoa maoni, wajumbe wa kamati wamepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na wizara ikiwemo taasisi zake ambapo Mjumbe wa Kamati Mhandisi Stella Manyanya ameishauri Taasisi ya Jilolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuangalia uwekezano wa kufanya tafiti ambazo zitasaidia kubaini uwepo wa madini katika halmashauri ambazo hazinufaiki na mapato yanayotokana na shughuli za madini ili kuziwezesha halmashauri hizo kunufaika na rasilimali hiyo kama zilivyo nyingine.
Mbali na kamati hiyo, kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo, Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Taasisi chini ya Wizara na Wataalam kutoka wizarani na taasisi zake.