Breaking

Friday, 30 September 2022

DKT. KIRUSWA ATAKA KUANZISHWA KITUO CHA UNUNUZI WA MADINI IGUNGA



Na Asteria Muhozya, Igunga

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemwagiza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora kuanza mchakato wa kuanzisha Kituo cha Ununuzi wa Madini katika Wilaya ya Igunga ili kurahisisha biashara ya Madini katika Wilaya hiyo inayoongoza kwa uzalishaji wa madini mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora inabainisha kuwa, Wilaya ya Igunga ndiyo inayoongoza katika uzalishaji wa dhahabu mkoani humo ikifuatiwa na wilaya ya Nzega, Sikonge na Kaliua.

Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa, mzunguko wa fedha katika soko la madini Tabora umefikia shilingi bilioni 48 zinazotokana na biashara ya kuuza na kununua dhahabu inayofanywa na wafanyabiashara 17 waliopo katika soko kuu la mkoa ambao wanategemea dhahabu inayozalishwa na wachimbaji wadogo kutoka wilaya za mkoa huo.

Kufuatia mafanikio hayo na kutokana na mwenendo mzuri wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali, Dkt. Kiruswa ametoa siku 90 kwa Afisa Madini Mkazi kuhakiki na kuwasilisha wizarani taarifa za walio hodhi leseni zao bila kuziendeleza kwa kipindi kirefu ili maeneo hayo wapatiwe watu wengine wenye nia ya kuwekeza.

Vilevile, katika jitihada za kuendelea kuwawekea wachimbaji mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao kwa tija, Dkt. Kiruswa amezitaka Taasisi za Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufika mkoani humo kuangalia eneo ambalo linaweza kutumiwa kwa uwekezaji wa mtambo wa kuchenjua marudio ya dhahabu suala ambalo wachimbaji wameiomba Serikali kuliangalia.

Ameongeza kwamba, wizara imeweka mpango kabambe wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kuhakikisha wanachimba bila kubahatisha kwa kuiwezesha STAMICO kuja na mkakati wa kununua mtambo wa uchorongaji kwa ajili shughuli za wachimbaji wadogo.

" Tunataka kuona wachimbaji wadogo wanachimba kwa tija na wanakua kutoka kwenye uchimbaji mdogo," amesema Dkt. Kiruswa.

Kadhalika, ameendelea kusititiza suala la wachimbaji wadogo kujiunga katika vikundi ili kupata huduma kwa urahisi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amewapongeza wachimbaji wadogo Daudi Mwita mmiliki wa kampuni ya Kasala Gold Limited na Meneja Mkuu wa Kampuni ya TAUR Tanzania Limited kutokana na uwekezaji mkubwa walioufanya ikiwemo kufanya uchimbaji wa kisasa, uwekezaji kwenye jamii na kutoa nafasi kwa wachimbaji wengine kukua na kujipatia vipato.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Mayigi Makolobela amewataka wachimbaji kutunza takwimu zao za biashara ikiwemo taarifa za uzalishaji na kufuata mfumo rasmi wa kibiashara wa Serikali ili iwe rahisi kukopeshwa na taasisi za fedha.

Ameongeza kuwa, Ofisi yake itaendelea kutoa elimu kuhusu kuingia makubaliano ya kibiashara, uchimbaji salama na wenye tija, pamoja na mambo mengine yanayohusu sekta hiyo.

Ameendelea kuwasisitiza wachimbaji kupima madini na kaboni zao kwa kina kabla ya kuchenjua ili kuepusha malalamiko ya kuibiwa katika viwanda vya kuchenjua dhahabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo amezipongeza kampuni za TAUR Tanzania Limited na Kasala Gold Limited kutokana na uwekezaji uliofanywa kwenye wilaya hiyo ikiwemo huduma za kijamii ambazo kampuni hizo zimechangia kwa jamii.

Ziara ya Naibu Waziri ililenga kuangalia maendeleo ya shughuli za wachimbaji mkoa wa Tabora, kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wachimbaji ikiwemo mwenendo wa Sekta ya Madini mkoani humo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages