Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo leo Septemba 27, 2022 wametembelea banda la Tume ya Madini kwenye Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.
Mara baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalam wa Tume ya Madini, Naibu Katibu Mkuu ameitaka Tume ya Madini kuendelea kutoa elimu hasa katika eneo la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ili wananchi wengi waweze kushiriki kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini na kujipatia kipato huku Serikali ikipata mapato yake.
" Wananchi wengi bado wanahitaji elimu kuhusu fursa zilizopo kwenye migodi ya madini na kuanza kutoa huduma kama vile vyakula, ulinzi n.k," amesema Mbibo
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo ameitaka Tume ya Madini kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini ili kuzuia migogoro kati ya wananchi na wawekezaji kwenye shughuli za madini.
"Mnafanya kazi nzuri sana lakini ni vyema mkaweka nguvu zaidi kwenye utoaji elimu kwa wawekezaji na wananchi wanaomiliki mashamba ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa shughuli za uchimbaji wa madini," amesema Shimo