Breaking

Thursday, 8 September 2022

CHELSEA YAPATA MRITHI WA TUCHEL



Na Said Muhibu,LLH

Klabu ya Chelsea imefanikiwa kupata saini ya Kocha wa Brighton & Hove Albion Graham Potter kwa kandarasi ya miaka mitano kurithi kiti cha Thomas Tuchel ambaye ametimuliwa hapo jana.

Potter ambaye amekuwa na mwenendo mzuri akiwa Mkufunzi wa Brighton ataanza kukinoa kikosi cha Chelsea mara moja baada ya utambulisho wake.

Raia huyo wa Uingereza mwenye miaka 47 amesema anafurahi sana kujiunga na Chelsea huku akitarajia kuifanyia mambo makubwa klabu hiyo.

“Ninafuraha kujiunga na Chelsea, klabu bora kabisa, nina shauku ya kufanya kazi na wamiliki wa klabu hii kwa kushirikiana vizuri na kuimarisha kikosi hiki,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti na Mmiliki Mkuu wa Chelsea Todd Boehly amesema kuwa Potter ndiye chaguo sahihi katika mipango yake ya kuinoa na kuikuza klabu hiyo huku akitarajia makubwa kutoka kwake.

“Tunayo furaha kumleta Graham ndani ya klabu ya Chelsea, ni kocha tunayemuamini na mbunifu ndani ya ligi kuu nchini Uingereza, ana ujuzi na uwezo wa kuipa maendeleo klabu yetu,” alisema Boehly.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Brighton, Potter ametua Chelsea na kikosi kazi chake akiwamo msaidizi wake Billy Reid, kocha wa kikosi cha kwanza Bjorn Hamberg na Bruno, kocha wa makipa Bem Roberts na Mkuu msaidizi wa kuajiri Kyle Macaulay 

Potter anasifika kwa kutengeneza timu inayoshambulia zaidi akitumia staili ya kipekee ya umiliki wa mpira na kupiga pasi nyingi. Akiwa na Brighton kwa misimu mitatu amefanikiwa kumaliza nafasi ya 15 kwa mwaka 2019/20, nafasi ya 16 kwa mwaka 2020/21 na nafasi ya 9 msimu uliopita.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages