Na OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa, amewahimiza Wakulima mkoani Kagera kuendelea kulima kahawa kwa kuwa zama za bei kandamizi zimeisha chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan
Bashungwa ametoa kauli hiyo Septemba 10, 2022 alipokuwa akitoa salamu za serikali kwa wananchi wa Wilaya Kyerwa kwenye Dua maalum iliyoandaliwa na familia ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, AbdulMajid Nsekela.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kuimarisha mifumo ya manunuzi ya kahawa ili misimu ijayo bei iendelee kuongeza na kuwa na ushindani.
“Tunataka mkulima anufaike na jasho lake, endeleeni kulima kwa sababu zama za kukata tamaa kwa sababu ya bei kandamizi ambayo haiwanufaishi wakulima zimeisha chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa alieleza hatua za utekelezaji wa miradi ya Barabara ya Nyakahanga mpaka Benako, Barabara ya Bugene mpaka Kyerwa na Barabara ya Omugakorongo hadi Murongo ambazo zote zinawekewa lami na zitafungua uchumi wa Wilaya ya Kyerwa kwa kuunganishwa na nchi jirani.
Vile vile, amebainisha mipango ya serikali ya kuboresha sekta za afya na elimu ambapo serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba nchi nzima na kwa upande wa elimu itaendelea kutolewa bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita.
Dua hiyo Maalum iliongozwa na Mufti na Shekhe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi aliyeambana na viongozi mbalimbali wa dini na serikali, nyumbani kwa Mkurugenzi wa CRDB.