Breaking

Thursday, 15 September 2022

DKT. ABBAS AIPA IDARA YA MICHEZO SIKU 7 KUKAMILISHA NYARAKA ZA MIRADI



Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ametoa siku 7 kwa watendaji wa Idara ya Michezo kukamilisha nyaraka za miradi yote iliyoko chini ya Idara hiyo la sivyo kila mhusika atabeba mzigo wake.

Dkt. Abbasi ametoa agizo hilo leo Alhamisi September 15, 2022 alipokutana na watendaji wote wanaosimamia sekta ya michezo nchini kuanzia Idara ya Maendeleo ya Michezo iliyoko Wizarani, Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na Baraza la Michezo (BMT).

“Kuna changamoto kubwa sana za kiutendaji zilizobainika katika Idara ya Maendeleo ya Michezo kiasi cha kukwamisha miradi mingi nimekuja kuwaambia hapa nyie ndio wataalamu sisi tunatafuta hela kuna mabilioni ya fedha Serikali imetenga kila nyaraka unayouliza kazi zianze unaambiwa bado, kila kitu unachohitaji ukapewe hela Hazina hakijaandaliwa, sasa tumefanya mabadikiko ya uongozi wa juu wa Idara hii tunataka sasa kazi na matokeo na sio blah blah nyingi,” alisema Dkt. Abbasi.

Mtendaji Mkuu huyo wa Wizara ametoa siku saba kwa watendaji wanaokaimu katika Idara hiyo kukamilisha nyaraka hizo ikiwemo miradi ya ujenzi wa viwanja vya kupumzika wananchi, shule 56 za michezo na ukarabati wa viwanja mbalimbali vya michezo.

“Serikali inataka kazi na matokeo miradi yote hii mingi ishatengewa fedha na mingine tunahitajika kupata maandiko yenu wataalamu lakini kwa kiasi kikubwa imekuwa stori nyingi tu. Sasa baada ya siku 7 hizo kila atakayekwamisha tutampa jukumu analoonekana analiweza zaidi na si katika Idara hii muhimu kwa nchi ya maendeleo ya michezo,” alisema.

Wakati huo huo, Dkt. Abbasi jioni hii amefanya ziara ya kustukiza kwenye Baraza la Michezo nchini kukagua utekelezaji wa maelekezo ya kulitaka Baraza hilo kununua vitendea kazi mbalimbali vya kisasa yakiwemo magari kwa ajili ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages