Breaking

Thursday, 29 September 2022

WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA CHANGAMOTO ZA WALIMU WA AJIRA MPYA KUFANYIWA KAZI



Eliud Rwechungura - Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amemwagiza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde kufuatilia Malalamiko na changamoto zote zinazowakabili Walimu wa Ajira Mpya 9,800 ili ziweze kufanyiwa kazi.

Ametoa maagizo hayo Septemba 28, 2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu nchini na kuagiza kufuatiliwa Malalamiko yote ambayo amekuwa akipokea kutoka wa Walimu wa Ajira Mpya zilizotolewa na Serikali mwezi Juni, 2022

Bashungwa amesema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa Walimu wa Ajira Mpya ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa baadhi ya wilaya ambazo hazijatoa fedha za kujikimu kwa Walimu hao.

Aidha, Bashungwa ameagiza kutolewa kwa ufafanuzi wa viwango vya malipo kwa mujibu wa tararibu na vigezo vinavyotumika katika malipo hayo ili kuondoa sintofahamu ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita ni sikivu na itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto watakazokumbana nazo Wakati wakitekeleza Majukumu ya kuwafundisha wanafunzi.

Ikumbukwe kuwa tarehe 26 Juni, 2022 Seikali ilitoa ajira za kada za ualimu kwa waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo 9,800 ambapo walimu 5,000 wamepangwa shule za Msingi na walimu 4,800 shule za sekondari.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages