Na Said Muhibu, Lango la Habari
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani mauaji ya watu watatu, Mairo Togoro (56), Mwise Simon (54), na Mugare Mokiri waliotuhumia kujihusisha na ujambazi wilayani Serengeti Mkoani Mara usiku wa kuamkia Septemba 22 majira ya saa 8 usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho Benson Kigaila, amesema kuwa kitendo cha jeshi la polisi kuwauwa watuhumiwa hao kinakiuka sheria za nchi hii.
Kigaila amesema kuwa uchunguzi wao ulibaini kuwa idadi ya watuhumiwa wa ujambazi waliokamatwa ni tofauti na iliyotajwa na RPC wa Mara, na kuongeza kuwa watuhumiwa hao wanne hawakufikishwa kituo chochote baada ya kukamatwa.
“Waliwakamata majira ya saa 12 alfajiri na wanakijiji wote wanajua, wanakijiji wakawa wanawashangaa kwasababu sio watu majambazi, wakawafuatilia kituo cha polisi hawakuwakuta”
“RPC anasema waliuawa saa 8 usiku wa kuamkia tarehe 22, hivyo wamekaa nao zaidi ya masaa 20, kwa maelezo ya OCD wa Serengeti hakukuwa na kituo chochote cha polisi ambacho hawa watu waliokamatwa walikuwa wameandikishwa kuwa wamefikishwa pale,” alisema Kigaila.
CHADEMA imedai kuwa jeshi la polisi liliwakamata watu zaidi ya wanne kwenye operesheni iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya jeshi la polisi Mkoa wa Mara, Mwanza, Simiyu na Tarime kufuatia matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yanayodaiwa kufanywa katika maeneo hayo.
“Walikamata watu wengi sana lakini wengi waliwaacha baada ya kuwadai fedha kuanzia Milioni 1 hadi 2 na nusu, na walioachiwa wapo tayari kutoa ushahidi ila hawa wanne ndo hawakutoa hiyo fedha kwa njia ya miamala ya simu na ushahidi tunao”
“Na ndio maana hayo masaa 20 yote walioyokuwa wamewashikilia hao watu wanne hawakuwasajili kituo chochote cha polisi, walikuwa nao muda wote wakidai fedha,” alisema Kigaila.
Septemba 22 mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP Longinus Tibishiwanu alithibitisha kutokea kwa mauaji ya watu watatu huku mmoja akikimbia baada ya kujaribu kuwatoroka askari usiku wa kuamkia tarehe 22 mwezi huu.
RPC Tibishiwanu alisema kuwa watu hao walikiri kuhusika na matukio ya ujambazi baada ya kufikishwa kituo cha polisi na wakawataja wenzao watatu waliokuwa wakishirikiana nao.
“Usiku watuhumiwa hao waliwaongoza polisi Kwenda kuwaonyesha walipojificha wenzao watatu, lakini walipofika Kitongoji cha Gentamome majira ya saa 8 usiku ghafla askari hao walishambuliwa na risasi kutoka porini nao wakajibu mapigo,” alisema RPC Tibishiwanu.
Akizungumza kwa njia ya simu na Lango la habari RPC Tibishiwanu amekanusha madai ya CHADEMA na kuongeza kuwa askari walifanya kazi yao kwa mujibu wa sheria.
"Askari wetu walifanya kazi yao kwa weledi, haki na kuzingatia sheria kwa hiyo hayo wanayoyasema si ya kweli," alisema RPC Tibishiwanu
Aliongeza kuwa hakukuwa na askari yeyote aliyedai fedha kwa watuhumiwa hao kama ilivyoelezwa na CHADEMA huku akisisitiza kuwa wakazi wa Nyamwihuru ambapo tukio la mauaji lilitokea wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuondoa uhalifu huo.
"Kazi ilifanyika kwa umakini na weledi na ukienda hapo kijijini watu wanafurahi na kulipongeza jeshi la polisi kwa kuondoa uhalifu huo, lakini watu hawalizungumzii hilo wanakalia lawama tu," alisema.
Hata hivyo CHADEMA imemuomba Rais Samia Suluhu Hassa kuwaondoa baadhi ya viongozi wanohusika na vyombo vya dola pamoja kuunda Tume huru ya kijaji ili kuchunguza ukweli wa mauaji hayo na kuthibitisha usahihi wa kile kilichosemwa na chama hicho.
“Tunamtaka Rais Samia amuondoe IGP Wambura, DCI Kingai, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara na Kamanda wa Polisi wilaya ya Serengeti,” alisema Kigaila.