Na Said Muhibu,LLH
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi juu ya kufilisika kwa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kabla ya kujadiliwa kwa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa watu wote Bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya maazimio ya Kikao cha Kamati Kuu ya Chama hiko kilichofanyika Septemba 17-18, Mjumbe wa Kamati Kuu na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar Salum Mwalimu amemuomba CAG kufanya ukaguzi maalum juu ya kufilisika kwa NHIF na kuja na ripoti itakayoonesha tathmini juu ya jambo hilo.
"Kamati Kuu inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum kwenye Mfuko wa Bima ya Afya Nchini na kutoa taarifa yake kwa umma kuhusu mwenendo wa hali ya Mfuko wa fedha za wanachama wa mfuko huo ikiwa ni pamoja na Madeni yake," alisema Mwalimu.
Mwalimu ameongeza kuwa suala la Afya ni nyeti sana kwa maslahi ya Taifa, huku akiiomba serikali iwe na uwazi juu ya kufilisika kwa Mfuko wa Bima ya Afya Nchini (NHIF).
"Suala sio tunaaambiwa tu mfuko upo kwenye hali mbaya, tuambieni kilichotufikisha huko ni nini?" alihoji Mwalimu.
Aidha, Mwalimu ameiomba Serikali kutoa muda wa kutosha ili kujadili kwa kina juu ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa watu wote kabla ya kujadiliwa Bungeni na kupitishwa kuwa Sheria.
Ameongeza kuwa Serikali isitumie utaratibu wa hali ya dharura kuharakisha upitishwaji wa Sheria hiyo kabla ya kujadiliwa kwa kina juu ya Muswada wake.
"Kamati Kuu imeitaka Serikali kutoa muda wa kutosha kujadili Muswada wa Sheria mpya ya Bima ya Afya kwa watu wote badala ya kutumia utaratibu wa hali ya dharura"
"Tumeisikia Serikali inataka kutumia utaratibu wa hati ya dharura kutaka kupeleka muswada huo Bungeni, tusingeshauri, tunakataa na tunapinga CHADEMA hati ya dharura," akisisitiza Mwalimu.
Mnamo Agosti 11 mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji wa NHIF Bernard Konga alisema kuwa kuna udanganyifu mwingi unaofanywa na watoa huduma wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa, hali inayouumiza mfuko huo lakini wanapambana na hali hiyo.
"Udanganyifu upo na tumekuwa tukichukua hatua, tutasitisha mikataba itakayoonekana inahatarisha uendelevu wa mfuko. Tumekuwa tukichukua hatua ikiwamo kupiga faini, kuwaripoti wahusika katika mabaraza yao kuhakikisha tumelipia huduma halali kulingana na miongozo,” alisema Konga.
Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mashirika ya umma ya Machi 2022, ilionyesha NHIF ilipata hasara ya Sh109.71 bilioni.
Katika Maazimio mengine CHADEMA iliiomba Serikali ifanye marekebisho ya Sheria ya fedha ya 2022/2023 iliyopitisha utozaji wa tozo, kuja na mikakati mipya kukabiliana na kupata bei za nafaka na Mafuta, kurekebisha sheria inayopinga mikutano ya hadhara kwa vyama pinzani vya siasa.