WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inasimamia kikamilifu sekta ya nishati ikiwemo kuendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania ili kukuza uchumi.
“Mradi huu ni muhimu kwa manufaa ya nchi zetu mbili katika kukuza biashara, viwanda vya uzalishaji, kuongeza ajira pamoja na kuvutia wawekezaji ambao wanatarajia kukuza teknolojia na ujuzi kwa wananchi. Mheshimiwa Rais ana matamanio makubwa ya kuifanya sekta ya nishati kuwa chanzo cha ukuaji wa uchumi na kuboresha sekta nyingine ikiwemo viwanda ambavyo ukuaji wake unategemea zaidi uwepo wa nishati ikiwemo mafuta na gesi.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Ijumaa, Septemba 23, 2022 wakati akiahirisha mkutano wa nane wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Amesema baadhi ya wadau wa maendeleo wamekuwa na mashaka katika utekelezaji wa mradi huo wakihofia kuwa unaweza kutekelezwa pasipo kuzingatia athari za kimazingira na haki za binadamu.
Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza mradi huo umefanyiwa tathmini ya kina ya kimazingira na kuhakikisha kuwa utekelezaji wake hauna athari za kimazingira na kwa jamii. “Mradi huu kwa upande wa Tanzania unagusa watu 9,513 ikiwemo taasisi mbalimbali. Miongoni mwao ni watu 331 pekee ndio watakaohamishwa sawa na asilimia 3.5.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa wanaoguswa na mradi huo walishirikishwa kuchagua kujengewa makazi mapya au kupewa fedha taslimu. Hata hivyo asilimia 85 walichagua kujengewa makazi na ujenzi wa makazi hayo unaendelea ambapo nyumba 37 kati ya 309 zimekamilika na kukabidhiwa kwa wahusika. Aidha, nyumba 55 zipo kwenye hatua ya umaliziaji na nyumba 217 zipo kwenye hatua za awali za ujenzi.
Amesema Serikali ya Tanzania inaungana na Serikali ya Uganda kuwahakikishia wadau wote likiwemo Bunge la Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kimataifa kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia sheria zote za Tanzania na za Kimataifa, uwazi, tahadhari za kimazingira, ulinzi wa mifumo ya kiikolojia na rasilimali za maji, masuala ya kijamii, kijinsia na haki za binadamu kwa ujumla.
“Hivyo niwatoe hofu wadau wote kuhusiana na utekelezaji wa mradi huu na Serikali itaendelea kutumia njia za kidiplomasia kuhakikisha wadau wanapata taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa mradi na uzingatiaji wa viwango vya Kimataifa.”