Mwalimu wa shule ya msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Mbuje iliyoko wilayani Rungwe, mkoa wa Mbeya, Saimon Mtambo (44) amemcharanga mapanga mke wake Fortunata Abraham (36), na watoto wake wawili kisha na yeye kunywa sumu na kupoteza maisha chanzo kikidaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa.
Diwani wa Kata ya Kiwira, Michael Mwamwimbe, amesema huenda mauaji hayo yalitokea wiki tatu zilizopita na kwamba chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa ambao umedumu kwa muda mrefu.
Aidha Mwamwimbe amefafanua kuwa watoto waliocharangwa mapanga na kisha kufariki dunia ni kijana wa kidato cha kwanza shule ya sekondari ya wavulana Busokelo na mtoto wa darasa la nne aliyekuwa anasoma shule ya msingi Ikuti iliyoko jijini Mbeya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Dkt. Vicent Anney, amesema kuwa miili ya watu hao wanne imekutwa imeharibika na watazikwa kesho Septemba 15, 2022.
Source: EATV